Serikali ya kaunti ya Mombasa imeahidi kushughulikia matakwa na lalama za maskwota wanaoishi katika ardhi zenye utata na migogoro.
Akizungumza na maskwota hao walipowasilisha lalama zao nje ya majengo ya bunge la kaunti, Waziri wa Ardhi na Mipangilio ya Mji kaunti ya Mombasa Mohamed Hussein ‘Amadoh’ amewahakikishia kuwa serikali ya kauti hiyo inawajibikia lalama zao kwani tayari Bunge la kaunti limepitisha sheria ya ugavi wa ardhi.
Amadoo amesema serikali ya Kaunti ya Mombasa inapania kuzinunua ardhi hizo zenye utata na mizozo na kuwakabidhi kupitia kwa sheria hiyo, kufikia mwishoni mwa mwezi Januari.
“Shida hizi hazikuanza jana na juzi bali zimekuwepo tangu zama za babu zetu.Tumetafuta suluhu ya jambo hili kwa muda mrefu mpaka leo mheshimiwa gavana ametuletea sheria ya kutatua hili janga.Tafadhalini nawaomba tuwe na subira hii shida itatulike hapa Mombasa,” alisema Amadoh.
Kwa upande wake Seneta mteule wa Mombasa Miraj Abdillahi ambaye amekuwa mstari wa mbele kupigania haki za maskwota dhidi ya kunyakuliwa ardhi zao na mabwenyenye, amewasihi waathiriwa hao wa mizozo ya ardhi kuwa watulivu huku viongozi wa idara husika serikalini wakishughulikia kilio chao.
“Hakuna mtu anayenunua shamba la babau yake .Yote yaliyoandikwa katika petition ni ya kweli na nimesikia vilio vyenu, ila hamaki haitatua mambo.’’ Seneta Miraj alisema.
Maskwota hao wanalalamikia kuhangaishwa na baadhi ya mabwenyenye wanaolenga kuwafurusha katika ardhi hizo wanazoishi kutokana na mzozo wa umiliki sasa wakiililia serikali ya kaunti na ile ya kitaifa kuingilia kati kusuluhisha migogoro hiyo.
Haya yanajiri huku suala la mashamba bado likisalia tatizo sugu Kwa wakaazi wa Mombasa ambao mapema Jumaano waliandama na kukita kambi nje ya ofisi ya Gavana wakitaka majibu ya masaibu yanayowasibu.
By Mjomba Rashid