Viongozi wa upinzani wameendelea kuikashifu Serikali ya Kenya Kwanza kuhusu visa vya utekaji nyara vilivyoshuhudiwa nchini, sasa wakishinikiza kujiuzulu kwa rais William Ruto.
Kalonzo Musyoka wa chama cha Wiper amemshtumu Rais Ruto akidai kuhusika kwake kikamilifu na wimbi la visa vya utekaji nyara wa hivi majuzi na visa ambavyo viliathiri pia wakuu wa kisiasa kama vile Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi ambaye mwanawe alitekwa nyara na baadaye kuachiliwa..
“Suluhu pekee ni Rais William Ruto kujiuzulu. Ulimwengu umebadilika, na watu lazima wawajibishwe, jambo ambalo vijana wa Gen Z wanalishinikiza,” akasema.
Kalonzo alihoji jinsi Waziri Muturi, ambaye yuko katika Baraza la Usalama la Kitaifa, alivyopitia taabu zote za kumtafuta mwanawe, na jinsi mwananchi wa kawaida asiye na uhusiano na viongozi wenye ushawishi mkubwa wa kisiasa serikalini atakavyopata usaidizi.
“Muturi alisema amekuwa akingoja majibu kwa muda wa miezi sita kuhusu kilichompata mwanawe. Kinachofaa kuwatia wasiwasi Wakenya ni kwamba anaketi katika Baraza la Usalama la Kitaifa, na hili linafaa kuwa jambo la kutia wasiwasi sana sisi sote.” Akasema.
Kalonzo aidha alisema Mkurugenzi wa Idara ya Ujasusi nchini NIS, Noordin Haji hapaswi kuwajibishwa peke yake kwa visa hivyo kwani Rais Ruto kama kiongozi anapaswa kuwajibikia hayo.
Kulingana na Kalonzo, hatua kama hizo za utawala wa Ruto zinafaa kuchunguzwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Jinai (ICC), huku akishinikiza kuachiliwa mara moja kwa Wakenya waliotekwa ambao wamesalia kutojulikana waliko.
“Tumegundua kuwa mkuu wa kikosi hiki cha utekaji nyara yuko Ruaraka. Udikteta wa Rais Ruto na washirika wake lazima uchukuliwe kama kesi iliyoidhinishwa na mahakama ya ICC. Lawama hazitokani na mkuu wa DCI bali Rais Ruto,” akaongeza Kalonzo.
Ni kauli iliyoungwa mkono na Katibu Mkuu wa chama cha Jubilee, Jeremiah Kioni ambaye amesisitiza kuwa ni wakati mwafaka kwa Wakenya kumkamata rais Ruto kutokana na hali ya kutoridhishwa na utawala wake.
Huku hayo yakijiri chama cha Wiper kimetangaza kuondolewa kwa Mbunge wa Daadab Farah Maalim kama Naibu Kinara wa Chama cha Wiper kufuatia kauli yake kwa wanaomkosoa Rais Ruto.
By Mjomba Rashid