Aliyekuwa Waziri wa Jinsia na Turathi Aisha Jumwa na Seneta Mteule wa zamani Millicent Omanga wamepata nafasi mpya za kazi serikalini katika awamu ya hivi punde ya uteuzi.
Katika notisi ya gazeti la serikali iliyotolewa Ijumaa, Rais William Ruto alimteua Jumwa kuwa Mwenyekiti asiye Mtendaji wa Bodi ya Barabara nchini kwa muda wa miaka mitatu.
Jumwa, ambaye alifutwa kazi kama Waziri mnamo Julai mwaka jana, sasa anachukua nafasi ya Ahmed Kolosh Mohamed ambaye uteuzi wake umekatishwa.
Rais pia amemteua George Wanga kuwa Mwenyekiti asiyekuwa Mtendaji Mamlaka ya Kudhibiti Kawi na Petroli (EPRA) kwa kipindi sawia na hicho, akichukua nafasi ya Jackton Boma Ojwang ambaye muda wake wa kuhudumu sasa umebatilishwa.
Waziri wa Ulinzi Soipan Tuya alimpendekeza Seneta wa zamani Omanga kama mwanachama wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kenya Shipyards Limited kwa muda wa miaka mitatu, kuanzia Jumanne, Januari 14.
Allan Kosgey, ambaye mnamo 2022 aliwania ugavana wa Nandi katika chama cha UDA lakini akashindwa na Gavana wa sasa Stephen Sang wakati wa mchujo, pia amepata kazi kama Mwenyekiti asiyekuwa Mtendaji wa Bodi ya Taasisi ya Mali ya Viwanda ya Kenya kwa muda wa miaka mitatu.
Uteuzi wake Kosgey umetekelezwa na Waziri mpya wa wa Biashara Lee Kinyanjui saa chache tu baada ya kushika wadhifa huo.
Rais Ruto hakukomea hapo Katika tuezi hizi za nyadhfa za kazi, amemteua Mary Wanjira Kimonye kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) kwa muda wa miaka 6 na aliyekuwa Kamishna wa IEBC Boya Molu kama mmoja wa wanachama saba wa bodi ya Serikali kwa muda huo huo.
Wanachama wengine sita walioteuliwa katika tume hiyo: Harun Maalim Hassan, Mwanamaka Amani Mabruki, Francis Meja, Dkt. Irene Cherotich Asienga, Joan Andisi Machayo na Dkt. Francis Otieno Owino.
By Mjomba Rashid