Maafisa waliohudumu katika serikali ya kaunti ya Tana River na wengine wanaohudumu kwa sasa waliokamatwa na tume ya kukabili Ufisadi nchini EACC wamekana mashtaka ya ufisadi yanayowaandama.
Maafisa hao wanane waliofikikishwa kortini mjini Hola kaunti hiyo wanakabiliwa na mashtaka manane yakiwemo ukiukaji wa sheria za ununuzi kuhusu zabuni ya ujenzi wa ua wa KWS na sehemu za makazi za shirikia hilo mwaka kifedha 2016/2017 miongoni mwa makosa mengine.
Mbele ya Hakimu mkuu mwandamizi Edward Too washukiwa hao wanane ambao ni pamoja na Fatma Zahra, Abashora Swaleh Salad, Mohammed Naste, Ali Dida, Fatuma Napashe, Issa Funani na Kelvin Simiyu wamekana mashtaka yote manane yanayaowakabili huku washukiwa wengine 6 wakikosa kufika mahakamani.
Mahakama imewaachilia kwa dhamana ya pesa taslim shilingi 300,000 au dhamana ya shilingi laki tano na mdhamini wa kiasi sawia na hicho, huku hakimu Too akiagiza kesi hiyo kutajwa Januari 30 mwaka huu, na washukiwa hao wengine ambao hawakuwa mahakamani kuhakikisha wanafikishwa.
By Mjomba Rashid