HabariMombasaNews

Nitafika Mahakamani Muda Ukifika; Inspekta Jenerali Kanja Aahidi Kutii Maagizo ya Korti

Inspekta Jenerali wa polisi Douglas Kanja ametoa onyo kali kwa wahalifu wanaohusika katika visa vya utekaji nyara humu nchini.

Akizungumza huko Diani kaunti ya Kwale katika kongamano la kila mwaka la kutathimini utendakazi wa maafisa wa usalama wa ngazi za juu hadi zile za chini, Kanja amesema uchunguzi kuhusu visa hivyo ambavyo vimekuwa vikiripotiwa unaendelea huku akiahidi atakayepatikana atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka.

Kanja amesema kuwa yeye binafsi ametoa maagizo kwa idara ya upelelezi ili kuharakisha mchakato wa kutafuta majibu ya kitendawili cha visa hivyo kilichoibua ghadhabu na hofu miongoni mwa Wakenya.

Aidha Inspekta huyo amegusia swala la kukosa kufika mahakamani kwa mara tatu mfululizo akiwataka wakenya kuondoa hofu badala yake amesisitiza kuwa atafika mahakami wakati ukifika.

Itakumbukwa kuwa wiki iliyopita Mahakama ya Milimani jijini Nairobi ilimwagiza Inspekta Jenerali huyo na Mkuu wa Idara ya Upelelezi Mohammed Amin kufika mahakamani Alhamisi Januari 23 kubaini kitendawili cha wlaiko vijana watatu waliotekwa nyara.

Haya yanajiri huku Mkuu huyo wa Idara ya polisi akiahidi kufanya kazi na idara zote ili kuhakikisha kuwa maisha na usalama wa Wakenya yanapewa kipaumbele inavyostahili.

By Bintikhamis Kadide