AfyaHabariNews

Sekta ya Afya Nchini Kuathirika Pakubwa na Hatua ya Marekani Kujiondoa WHO

Wizara ya Afya imebaini kuwa sekta ya Afya itaathirika pakubwa na hatua ya taifa la Marekani kujiondoa katika Shirika la Afya Duniani, WHO.

Akizungumza hapa mjini Mombasa wakati wa Kongamano la Masuala ya Afya Afrika Mashariki, Waziri wa afya nchini Deborah Mulongo Barasa amekiri kuwa sekta ya afya itayumba kufuatia uamuzi huo wa Rais wa Marekani Donald Trump kuliondoa taifa hilo katika shirika hilo la Umoja wa Mataifa ikizingatiwa kuwa Marekani ni mchangiaji mkubwa wa WHO kwa kutoa ufadhili mkubwa wa kifedha ambao ni muhimu kwa oparesheni za WHO.

Serikali sasa imbioni kutafuta chanzo mbadala cha fedha baada ya uamuzi huo sawia na kutathmini maeneo ambayo yataathiriwa na kuondoka kwa Marekani.

Waziri Deborah amesema serikali ya Marekani imekuwa ikifadhili miradi kadhaa nchini na kuondolewa kwa misaada yake kutayumbisha pakubwa sekta ya afia nchini.

Hata hivyo waziri huyo amesema serikali inaendelea kuweka mikakati kabambe ikiwemo kutafuta pesa na mbinu mbadala za kukabili changamoto ambazo huenda zitatokana na hatua hiyo ya taifa la Marekani ya kujiondoa WHO.

Kwa upande wake Afisa wa masuala ya mauzo katika kampuni ya Safaricom Cynthia Kropac amesema kampuni hiyo pamoja na wadau wengine wataendelea kushirikiana kwa karibu na serikali kuu kuhakikisha kuwa sekta ya afya imeboreshwa nchini wakati huu inakabiliwa na changamoto chungu nzima za kifedha  na pia vifaa vya kisasa vya kufanikisha utoaji wahuduma za afia nchini.

Haya yanajiri huku WHO ikiendelea kutathmini hatua hiyo ya Marekani kujiondoa katika shirika hilo la Umoja wa Mataifa, uamuzi walioutaja wa kujutia na kutamausha.

Hata hivyo mbali na kujutia uamuzi huo wa Marekani Msemaji wa WHO Tarik Jasarevic alisema WHO inatarajia taifa hilo litazingtia upya uamuzi huo na wanatarajia kushiriki mazungumzo ili kuimarisha ushirikiano kati ya shirika hilo na Marekani.

Itakumbukwa kuwa Marekani ni mchangiaji mkubwa wa Shirika hilo lenye makao yake makuu mjini Geneva, Switzerland kwa kutoa ufadhili mkubwa wa kifedha ambao ni muhimu kwa oparesheni za WHO.

By Isaiah Muthengi