Kadri dunia inavyoendelea kupiga hatua katika utafiti, ndivyo vijana wanavyozidi kuonyesha juhudi katika kuvumbua mbinu mpya za kuboresha maisha yao na jamii kwa ujumla.
Javan Mghendi, ni mmoja wa vijana shupavu na hutumia ujuzi wake kubuni njia mbadala ya kutengeneza makaa kwa kutumia karatasi za kawaida, uvumbuzi unaomsaidia kupanua mawazo yake na kuongeza maarifa zaidi.
Akizungumza na Sauti ya Pwani, Mgendi alieleza kuwa alikuwa na kikundi cha vijana 15, ambao aliwapa mafunzo kuhusu mradi huo kwa lengo la kueneza maarifa na kuhakikisha kuwa uvumbuzi huo unazidi kushamiri miongoni mwa vijana wengine.
“Nilikaa na vijana 15 na kuwaeleza kuhusu ubunifu huu. Nashukuru walielewa na wakaamua kuuchukua na kuuboresha zaidi. Vilevile, nimeweka mikakati ya kuhakikisha mradi huu unaidhinishwa na taasisi husika kama Shirika la Mazingira la Neema ili kusaidia katika juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya tabianchi,” alisema Mgendi.
Mbali na kuendeleza utafiti wake, Mgendi alikuwa katika harakati za kutafuta uungwaji mkono kutoka kwa Shirika la Msalaba Mwekundu (Kenya Red Cross) na wadau wengine wa mazingira. Alisisitiza kuwa makaa aliyokuwa akitengeneza yalikuwa sawa kwa mazingira, kwani hayatoi moshi mwingi kama makaa ya kawaida yanayotokana na miti.
“Makaa haya ya karatasi ni mbadala mzuri kwa sababu hayachafui mazingira kama yale ya miti. Lengo langu ni kufanya utafiti zaidi ili kuona jinsi ya kuboresha zaidi mradi huu kwa kutumia malighafi nyingine rafiki kwa mazingira,” aliongeza Mgendi.
Mgendi alisema haya alipohudhuria kongamano lililowakutanisha vijana zaidi ya 300 katika kituo cha I.O.ME 001 chini ya Shirika la Msalaba Mwekundu mjini Mombasa. Kongamano hilo liliwaleta pamoja vijana kutoka maeneo mbalimbali ya Pwani kwa lengo la kujifunza na kushiriki katika miradi ya ubunifu.
Kwa upande wake, Fatma Yasin, msaidizi msimamizi wa vijana katika Shirika la Msalaba Mwekundu, alifurahishwa na jinsi vijana walivyojitokeza kwa wingi kupata mafunzo.
“Kongamano hili limewakutanisha vijana kutoka sehemu mbalimbali ili waweze kujifunza na kuona kwa macho miradi ya kibunifu iliyobuniwa na wenzao. Tunawahimiza vijana wakumbatie ujuzi wao na wajitengenezee fursa badala ya kujiingiza katika vitendo vya uhalifu,” alisema Yasin.
Wakati huo huo, Sophia Majid, mmoja wa vijana waliojitolea katika Shirika la Msalaba Mwekundu kwa zaidi ya miaka saba, alilisifia shirika hilo kwa mchango wake mkubwa katika kumjenga kitaaluma na kijamii.
“Nilianza kushiriki katika shirika hili tangu nikiwa shule ya upili, na kwa zaidi ya miaka saba nimepata mafunzo mengi, hususan katika nyanja za teknolojia na huduma kwa jamii. Hili limenipa motisha kuhakikisha kuwa kila ninachofanya kinawanufaisha watu wengi zaidi,” alisema Bi. Sophia.
Aliwahimiza vijana kutotumia muda mwingi nyumbani baada ya kumaliza masomo, bali wajihusishe na taasisi zinazotoa mafunzo ya kiujuzi kama Shirika la Msalaba Mwekundu, ambalo linaendelea kuwapa vijana fursa za kujifunza na kukuza vipaji vyao.
Kongamano hilo lilimalizika kwa mijadala yenye tija kuhusu ujasiriamali, uvumbuzi, na mchango wa vijana katika maendeleo ya jamii, huku wengi wakionyesha azma ya kuendeleza miradi waliyojifunza kwa manufaa yao binafsi na ya taifa kwa ujumla.
By Simon Cephas