Idadi ya watalii wa kigeni waliozuru taifa la Kenya mwaka wa 2024 imeripotiwa kuongezeka maradufu ikilinganishwa na mwaka wa 2023.
Hii ni licha ya hali ya taharuki na misukosuko ya kisiasa iliyokumba taifa kipindi cha mwaka uliopita wa 2024 ikiwemo ghasia na maandamano ya vijana wa Gen Z.
Akizungumza katika kongamano la kila mwaka la sekta ya utalii liloandaliwa mjini Mombasa, Waziri wa Utalii nchini Rebecca Miano ametoia ripoti akibainisha kuwa jumla ya watalii milioni 7.56 walizuru maeneo ya utalii nchini nchini.
Waziri Miano amesema watalii milioni 2.4 walikuwa wa kigeni huku milioni 5.1 wakiwa ni watalii kutoka humu nchini na kuongeza mapato ya taifa.
Waziri huyo kadhalika amesema sekta ya utalii nchini ilichangia pakubwa katika kapu la taifa huku akibainisha kuwa sekta hiyo ilikusanya shilingi Bilioni 452.2, ikiwa ni asimilia 19.7 zaidi ya kiwango cha pesa kilichokusanywa mwaka wa 2023.
Miano amesema tayari serikali kuu kupitia wizara yake na wadau wengine katika sekta ya utalii wameanza kuweka mikakati ili kuhakikisha kiwango hicho kimeongezeka kwa kiasi cha haja mwaka ujao.
“Mafanikio haya ya kimaendeleo yanatokana na uingiliaji kati wa kimkakati unaojumuisha kampeni kali za uuzaji, uboreshaji wa bidhaa za utalii, kupitishwa kwa mifumo ya kidijitali, na kuanzishwa kwa safari mpya za ndege zilizopangwa,” akasema Waziri.
Waziri Miano ametoa ahadi kwa wadau wote wa sekta ya utalii nchini kwamba serikali kuu kupitia wizara yake italendelea kushirikian nao ili kuafikia azima na malengo yao akisisitiza haja ya kuwepo wa mikahawa bora ya utalii, viwanja wa ndege na anga tua za kisasa nchini na uboreshaji wa maeneo mengine ya kitalii.
Katika ripoti hiyo, Marekani ingali inaongoza katika kundi la nchi lenye soko kuu la vyanzo vya mapato nchini Kenya, ikiwa na asilimia 12.8 ya wageni waliofika (wageni 306,501) huku Tanzania na Uganda zikifuatilia kwa karibu, zikichangia asilimia 8.4% na 9.4% mtawalia.
Kongamano hilo linajiri siku kadhaa baada ya meli mbili za watalii wa kigeni kutia nanga bandarini Mombasa mnamo siku ya Jumatatu.
Kuwasili kwa wakati mmoja kwa meli mbili za kitalii za MS Europa na MV World Odyssey ambazo zilikuwa na Zaidi ya abiria 1,600 na wafanyakazi kulipiga jeki utalii kaunti ya Mombasa na Kenya kwa jumla.
MS Europa, iliwasili Mombasa baada ya kutokuwepo kwa safari zake kwa muda wa muongo mmoja, ikiwasili kutoka Zanzibar ikiwa na watalii 334 na wafanyakazi 285 ndani yake.
Nayo meli MV World Odyssey, maarufu inayohusishwa na mpango wa ‘Semester at Sea’, ilitia nanga kutoka Cochin, India, ikiashiria ziara yake ya nne Mombasa. Meli hii, iliyobeba wanafunzi 677 na wahudumu 178.
By NEWS DESK