HabariNewsSiasa

Kinaya cha Kubana Matumizi! Ikulu, Afisi ya Rais na Naibu Wake Kupata Mgao zaidi wa Bilioni 4.8 za Bajeti ya Ziada

Imebainika kuwa Ikulu na afisi za Rais William Ruto na naibu wake Kithure Kindiki sasa zimetengewa shilingi bilioni 4.8 za ziada.

Haya ni kwa mujibu wa Bajeti ya Nyongeza ya II mwaka 2024/25 ambayo imewasilishwa mbele ya Bunge.

Data rasmi hizo zimeonyesha nyongeza hiyo ya ziada na kuibua maswali kuhusu hatua za kubana matumizi zilizotekelezwa ili kupunguza matumizi serikalini.

Hati hiyo ya Bajeti ya Nyongeza inaonyesha ongezeko la shilingi bilioni 86.18 la mgao katika mihimili mitatu ya serikali; Serikali Kuu Tendaji, Bunge na Mahakama.

Bajeti ya Ikulu iliongezwa kutoka shilingi bilioni 4.3 katika makadirio ya awali hadi shilingi bilioni 8.1 katika bajeti ya ziada chini ya mwaka wa kifedha wa 2024/25.

Sehemu kubwa ya gharama hizo ni kugharamia masuala ya baraza la mawaziri, mishahara, sherehe za kitaifa, uendeshaji na gharama za matengenezo kama vile bima ya matibabu.

Bajeti hiyo hata hivyo ni tofauti na Ofisi ya Utendaji ya Rais ambayo bajeti yake hugharamia utendakazi na matengenezo katika jumba la Harambee House.

Ofisi ya rais Ruto imetengewa shilingi milioni 651.7 za ziada; kutoka shilingi milioni 3.6.

Kutoka kwa bajeti ya ofisi ya Rais, shilingi milioni 615 zitaenda kwa huduma za uongozi, shilingi milioni 149 kwa huduma za kimkakati na sera.

Ofisi ya Naibu Rais Kindiki itapokea nyongeza ya jumla ya shilingi milioni 420 kwa mishahara, utendakazi, utawala mkuu, sera za kimkakati na masuala mengine.

Itakumbukwa kuwa kufuatia maandamano dhidi ya serikali yaliyofanyika Julai mwaka jana, Rais Ruto alitangaza hatua za kubana matumizi ili kurejesha pesa zitakazopatikana kutoka kwa Mswada wa Fedha wa 2024 uliotupiliwa mbali.

Tangu wakati huo, wakosoaji wametia doa na kukashifu hatua za kubana matumizi za rais Ruto wakidai rais anauma na kuvuvia kwa kutotenda kile anachokisema kutokana na kuongezeka kwa ukopaji na matumizi.

By Mjomba Rashid

Comment here