HabariNewsSiasa

Rais Ruto Awasuta Wakenya Wanaokejeli Ahadi yake ya kujenga Barabara ya Isiolo-Mandera

Rais William Ruto amewakashifu Wakenya ambao wamekuwa wakikejeli ahadi yake ya kujenga barabara ya Isiolo-Mandera yenye urefu wa kilomita 750.

Akizungungumza katika hafla ya Utiaji Saini wa Mkataba wa Uboreshaji wa Upatikanaji wa Umeme na usambazaji wa umeme mashinani kupitia Gridi ndogo na Mfumo wa Sola rais amebaini kujitolea kwa utawala wake kufanikisha mradi huo kwa wakati ufaao.

Kiongozi huyo wa taifa aliwakosoa vikali wakenya wanaotumia kauli yake ya barabara hiyo kama jambo la mzaha na kejeli akidokeza kuwa tayari mipangilio inaendelea ili kuhakikisha ujenzi huo wa barabara unakamilika.

Nilikuwa Kaskazini mwa Kenya, na nilitangaza muungano mkubwa wa barabara ambao utajengwa kutoka Isiolo kupitia Wajir, Mandera, na watu wengi wanafikiri ni mzaha. Katika nchi hii, wakati mwingine tunachukulia masuala ya maisha na kifo kana kwamba ni mzaha,” Ruto alisema.

Rais Ruto ameeleza kuwa kwa miaka mingi serikali imekuwa ikitelekeza maeneo ya kaskazini mwa Kenya kimaendelea akiahidi kuwajibika kwa mradi huo ili kuhakikisha wakazi wa maeneo hayo yananufaika kwa miradi ya serikali kama maeneo mengine.

Itambukuwa kuwa haya yanajiri wiki moja baada ya Rais alipokuwa ziarani eneo la Kaskazini mashariki kusema kuwa barabara hiyo yenye urefu wa zaidi ya kilomita 700 itashughulikiwa ili kuhakikisha hakuna mkenya anaachwa nyuma kwa maendeleo ya taifa.

“Tutatengeneza barabara itoke Mandera, ije Ramu, ije Garre, ije El-wak, ije Kobo, ije pale Kotulo, ije Tarbat, ipitie hapa Wajir, iende Samatan, iteremke Modogashe, ifike Isiolo, iende Nairobi,” Ruto alisema wakati wa ziara hiyo.

Ni kauli ambayo imezua gumzo na kusambaa mitandaoni huku Wakenya wakiifanyia stihizai na mzaha kwa kujirekodi na kutengeneza vichekesho maarufu memes, na video hasa katika mitandao ya Tiktok.

By Mjomba Rashid