Mashindano ya kimataifa ya ulengaji shabaha kwa kutumia bunduki (IDPA Africa Continenetal Championship) yameng’oa nanga rasmi katika klabu ya Bamburi Rifle, kaunti ya Mombasa.
Mashindano hayo yalianza kwa kishindo kikali jumla ya maafisa 36 waelekezi wa kiusalama wakishiriki katika vitengo mbalimbali vya ulengaji shabaha.
Mwenyekiti wa chama cha kitaifa cha wamiliki wa bunduki (NGOA) Sammy Onyango alisisitiza haja ya kuondoa woga unaoambatana na michezo hiyo akisema kwamba ni kama michezo mingine katika jamii.

Onyango alipuuzilia mbali kasumba ya kupotosha kuwa mchezo huo ni wa watu kutoka tabaka fulani la jamii na kusema kuwa mtu yeyote ana uwezo wa kushiriki.
“Mchezo wa ulengaji shabaha kutumia bunduki unaweza kumkuza mtu kama mchezo mwengine na kuna haja ya kufuta mawazo kwamba mchezo huu ni wa maafisa wa polisi au matajiri pekee.
Iwapo mtu anataka kujihusisha na mchezo huu anaweza kujiunga na vilabu kama vile klabu ya Bamburi Rifle ambapo atapata mafunzo yafaayo almraadi atatumia ujuzi huo katika nyanja ya michezo tu na sio kwa malengo mengine potovu,“ Onyango alisema.
Aliongeza kwa kuondoa hofu kuhusu hali ya usalama katika ukanda wa pwani kutokana na mchezo huo.
“Baadhi ya watu husema pwani ni eneo lenye hatari kubwa ya ugaidi lakini tunawaambia wote kwamba mchezo huu unaweza kufanyika maeneo haya katika mazingira maalum na salama yaliyotengwa.”
Onyango ambaye pia ni afisa mwelekezi wa kiusalama katika shirika la IDPA Afrika Mashariki na ya Kati aliyasifia mashindano na kuyataja kama njia mwafaka ya kukabiliana na changamoto ya msongo wa mawazo hasa kwa maafisa wa polisi.
“Kumekuwa na visa vingi vya msongo wa mawazo kwa maafisa wa polisi lakini kupitia kushiriki mchezo huu na sisi, wanaweza kukwepa mawazo na kuboresha afya yao ya akili huku wakiboresha ujuzi wao kwenye ulengaji shabaha,” Onyango alisisitiza.
Naibu Mwenyekiti wa klabu ya Bamburi Rifle Mohammed Ramadhan Swaleh kwa upande wake alitambua mashindano hayo kama chanzo muhimu cha kuboresha sekta ya utalii wa kaunti ya Mombasa na ukanda wa pwani kwa jumla.
Kulingana naye mashindano hayo yanayoleta pamoja walengaji shabaha kutoka maeneo mbalimbali ulimwenguni yatachangia katika ukuaji wa uchumi kwa kuleta biashara katika mahoteli pamoja na vivutio vya kitalii.
Zaidi ya hayo, Swaleh aliwahimiza wakaazi wa Mombasa kujitokeza kwa wingi kushudia mashindano hayo na kufichua kwamba klabu hiyo imeweka mikakati dhabiti kuhakikisha usalama wa mashabiki pamoja na kuwaandalia burudani mbalimbali.
“Tunatarajia kupata takribani mashabiki 150 na tumeweka mikakati ya usalama wao ikizingatiwa kwamb mchezo huu ni hatari na unaeweza kusababisha majeraha iwapo hatutaweka mikakati stahiki ya kiusalama.
Vile vile tumewaandalia burudani na tunataka wote watakaokuja hapa wafurahikie mashindano haya.” Swaleh alisema.
Mashindano hayo yatajumuisha divisheni 8, kila divisheni ikipangwa kulingana na silaha zitakazotumika huku washiriki wa kila divisheni wakigombania ubingwa wa divisheni yao na washindi wote wakipokezwa medali.
Vile vile mashindano hayo yalileta pamoja vitengo tofauti ikiwemo vile vya wanaume, chipukizi na hata wanawake.
Takribani walengaji shabaha 250 watashiriki mashindano hayo mwaka huu 50 kati yao wakitokea hapa Mombasa na waliobakia wakitokea maeneo mengine nchini na mataifa ya ughaibuni.
Tayari kufikia sasa timu kutoka mataifa ya Urusi,Romania, Estonia zilitua jijini Mombasa huku timu kutoka Italy ikitarajiwa kuwasili siku ya Ijumaa.
Aidha walengaji shabaha wa kibanafsi kutoka Zimbabwe na Africa Kusini pia waliwasili katika jiji hilo kuu la pili nchini Kenya tayari kwa mashindano hayo.
Haya ni makala ya nne ya mashindano hayo ya kimataifa ya Kiwango cha IV (Level IV) ambayo yanawaleta pamoja walengaji shabaha wanachama wa IDPA kutoka maeneo tofauti ulimwenguni.
BY MOHAMMED MWAJUBA