Hali ya usalama imetajwa kudorora katika kijiji cha Mnarani wadi ya Mnarani kufuatita kuibuka kwa magenge ya kihalifu yanayopora wakazi na kuwajeruhi kwa panga.
Magenge hayo ya kihalifu yanayojumuisha vijana wa kati ya umri wa miaka 16-21 yanadaiwa kuwapora na kuwajeruhi kwa panga wakazi wa eneo la Mnarani hali inayowafanya wakazi hao sasa kuishi kwa wasi wasi.
Wakiongozwa na Rukia Pamba Juma wakazi hao aidha wameeleza kuwa magenge ya vijana hao yamekuwa yakiwatishia dhidi ya kupiga ripoti kwa polisi wakiwaahidi kuwatoa uhai.
Wameongeza kuwa magenge hayo yamekuwa kwa kasi eneo hilo huku wakiwataka maofisa wa usalama kukabiliana na hali hiyo kwa haraka ili kusitisha uwezekano wa magenge hayo kujiunga na magenge ya vijana wahalifu kutoka maeneo mengine ukanda wa pwani na kutatiza zaidi wakazi.
“Utapata hao vijana hawana biashara, hawana chochote lakini kuna wakati tunashirikiana nao pamoja na mtu akidhulumiwa kama vile basi apige ripoti, angalau ile ripoti ikifika kituo cha polisi yule kijana ukimpata inakuwa rahisi kumshtaki. Lakini leo hii kijana kama yule amemnyang’anya mama simu ama kibeti, halafu anamuwekea panga anamwambia ukienda kuripoti naja malizana na wewe.” alisema Rukia.
Naibu kamishna eneo bunge la Kilifi kaskazini Samuel Mutisya Muinde amethibitisha kupokea taarifa ya uwepo wa magenge hayo akieleza kuwa mikakati ya kukabiliana na changamoto hiyo ya utovu wa usalama imewekwa.
Pia ametoa wito kwa wakazi na idara zote husika za serikali kushirikiana na maofisa wa usalama kwa kutoa taarifa zitakazo saidia kukamatwa kwa vijana hao.
“Tuko na changamoto ya kiusalama, tuko na changamoto ya vijana wadogo ambao wengine hawafuatilii masomo sana na kujiunga na kuwa wanasumbua watu. Na ile hatua ambayo tumefanya leo ni kutafuta ile kitu tunaita ushirikiano wa idara zote za serikali ili tupate kile tunachokiita “all government of one government approach”. alisema Mutisya.
Erickson Kadzeha