Vijana wahalifu kuchukuliwa hatua za sheria pamoja na wazazi wao Kilifi.
Kufuatia kushuhudiwa wimbi jipya la uhalifu unaohusisha magenge ya vijana ukanda wa pwani, onyo imetolewa kwa vijana wanaojihusisha na visa hivyo kwamba hatua za sheria zitachukuliwa dhidi yao na wazazi wao.
Takriban juma moja tu baada ya kuibuka kwa magenge ya vijana yanayotekeleza uhalifu katika wadi ya Mnarani, onyo kali imetolewa kuwa hatua za sheria hazitawasaza wazazi wa vijana wanaojihusisha na visa hivyo ili kuhakikisha kuwa usalama unadumishwa eneo hilo.
Kwa mujibu wa Warren Apopo ofisa wa kusimamia maswala ya watoto eneo bunge la Kilifi kaskazini ni kuwa wazazi wanajukumu la kuhakikisha wanakuwa na maadili mema hivyo basi hatua ya kuwachukulia hatua wote itapelekea kuwa waangalifu zaidi na wanao.
“Naomba mtuletee kwa ofisi tusaidie huyu mtoto tutampa ushauri nasaha ama ikiwezekana tutampeleka “approved”. Lakini mimi sitampeleka mtoto “approved” peke yake na niwache mzazi tunaelewana? Tufanya hivyo ili tuweze kumaliza hiki kisirani cha vijana kuwa na kiburi na kusumbua usalama katika jamii. Na wengine sasa wanavuta sigara, bangi na aina zote za dawa za kulevya.” alisema Apopo.
Kwa upande wake naibu kamshina eneo bunge la Kilifi kaskazini Samuel Mutisya Muinde amewarai wakazi na wadau mbali mbali kushirikiana ili kudumisha usalama.
Aidha ameongeza kuwa watahakikisha wamekabiliana vilivyo na magenge hayo ili wakazi wapate haki yao ya kuwa na usalama katika maeneo wanayoishi.
“Na pia ni kazi yetu kuhakikisha kuwa tumewapatia usalama wa kutosha na wao pia wanajukumu lao la kutimiza kwa kupeana ujumbe. Na sisi pia tutajikakamua tuhakikishe kwamba usaama umedhibitiwa. Na hilo tutafanya.” alisema Mutisya.
Erickson Kadzeha.