Athari za mabadiliko ya tabia nchi zikiendelea kushuhudiwa kila uchao kote ulimwenguni, mikakati inaendelea kuwekwa ili kukabiliana na athari za mabadiliko hayo.
Wadau na mashirika mbali mbali wamekongamana katika kijiji cha Mnarani kaunti ya Kilifi kuendeleza majadiliano ya kitaifa jinsi ya kunufaika na hewa kaa hususan ukanda wa pwani.
Kwa mujibu wa ofisa mkuu mtendaji wa taasisi ya utafiti wa samaki na viumbe wa majini nchini KMFRI Dkt. James Mwaluma mbinu ya kupanda mikoko na nyasi za baharini ni mbinu asilia za kutoa hewa kaa pamoja na kuwa mbinu ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
“Upanzi wa mikoko halafu pia njia nyingine ya uondoaji hewa kaa ambayo ni kupanda mwani maarufu nyasi za baharini “sea grass”. Lakini kwa upande wa mikoko ambao ndio mjadala wa leo kuna mbinu fulani ambazo zinaweza kutumika kutoa hewa kaa. Wanasayansi wa taasisi ya utafiti wa samaki na viumbe wa majini nchini KMFRI wamefanya huo utafiti wa majaribio katika kijiji cha Gasi kaunti ya Kwale nan i wazi kwamba mradi huu unafaida kubwa za kiuchumi na mazingira. Na kwa sasa hivi mbinu hiyo ya kutumia njia asilia za uondoaji hewa kaa umeenea tukisaidiwa na UNEP Go blue ambao ni wafadhili wetu katika mradi huu wa hewa kaa.” alisema Mwaluma.
Kauli hiyo imeungwa mkono na James Kairo mtafiti katika taasisi ya utafiti wa samaki na viumbe wa majini nchini KMFRI ameeleza kuwa mbinu mwafaka ya kukabiliana na athari hizo za mabadiliko ya tabia nchi ni kwa kutumia njia asilia kama vile upanzi wa mikoko, inayotoa takriban tani 1500 za hewa kaa kwa kila ekari moja ya mikoko.
“Ukiangalia vile kuna changamoto ya athari za mabadiliko ya tabia nchi, tunahitaji mazingira ambayo yataweza kuondoa hii hewa kaa. Hii ndio ile tunayoita “Nature based solution”. Kwa hivyo mikoko ikilindwa ni baadhi ya suluhu asilia ambayo itaweza kuzuia kwa kiwango kikubwa majanga yanayotukumba kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.” alisema Kairo.
Kwa upande wake mkurugenzi wa Jumuiya ya kaunti za pwani Dkt. Emmanuel Nzai ameeleza kuwa sheria na miswaada ya kutambuliwa kwa mikoko kama moja ya mimea muhimu yaani “cash crops” kama vile kahawa na majani chai inafaa kuundwa ili kunufaisha wakazi wa ukanda wa pwani.
“Ni kweli kabisa tukizungumza kuhusu mikoko, minazi, miembe tukizungumza haya yote ni kwamba yote ni mazingira ya pamoja na yote katika haya mazungumzo ya hewa kaa yanathamani kubwa katika ngazi zote hizi za hewa kaa. Kwa hivyo hii tukiangalia kwa sasa ndio kama raslimali yetu iko katika hewa kaa ambayo ni muhimu sana tuweze kuweka “policy” ya kuilinda.” alisema Nzai.
Ikumbukwe tayari baadhi ya wakazi katika maeneo ya Kwale na Lamu wamenufaika na mradi huo wa kutoa hewa kaa.
Erickson Kadzeha.