Takriban asilimia 21 ya watoto wa umri wa chini ya miaka mitano kaunti ya Kilifi hawakufanikiwa kuchanjwa chanjo muhimu za watoto mwaka 2024 hali inayopelekea watoto hao kuwa katika hatari ya kupatwa na maradhi kama vile kupooza na ukambi.
Idara ya afya kaunti ya Kilifi kupitia kitengo kinachosimamia chanjo imesema inaendeleza hamasa kwa jamii kuchanjwa ili kuwaepusha watoto hao kupatwa na maradhi ambayo yanaweza kuepukika kupitia kuchanjwa.
Kwa mujibu wa Christine Mataza muuguzi msimamizi wa shughuli za chanjo kaunti ya Kilifi licha ya kaunti ya Kilifi kupiga hatua na kuchanja watoto 46,000 kati ya 57,000 kungali na changamoto nyingi zinazochangia watoto kutochanjwa huku baadhi ya wakazi wakiongozwa na misingi ya dini isiyoruhusu wao kwenda hospitalini kupata matibabu wala chanjo.
Ameongeza kuwa kando na chanjo hizo kuokoa maisha ya watoto lakini pia zinasaidia miili ya watoto kujenga kinga ya zaidi ya asilimia tisini dhidi ya magonjwa.
“Huenda pia imani katika jamii yetu ya Kilifi kunazo dini ambazo haziruhusu watu kutumia “modern medicine” na hata chanjo pia ni kati ya “modern medicine”. alisema Mataza.
Atieno Joab daktari wa nyanjani katika kijiji cha Shingila wadi ya Sokoni anasema wamekuwa wakiripoti kwa maofisa wa polisi visa vya changamoto ya dini kutowaruhusu waumini wake kutafuta huduma za afya hospitalini, akitolea mfano kisa mjini Kilifi ambapo watoto wawili waliaga dunia nyumbani kwa kukosa matibabu.
“Kuna sehemu nyingine walikuwapo hata polisi ikahusishwa hapa Kilifi. Kulikuwa na watoto ambao walikuwa wanaugua labda ukambi ama sijui ni ugonjwa gani na watoto hao wawili wakaaga dunia nyumbani shauri dini yao ni ile ambayo watu hawaenda hospitali.” alisema Atieno.
Edward Mumbo mkuu wa kitengo cha afya ya msingi kaunti ya Kilifi anaeleza kuwa kitengo hicho hakijawezeshwa inavyofaa hivyo basi kutegemea kupata chanjo hizo kutoka kwa serikali kuu.
Hata hivyo ameweka wazi mpango wa kutumia madaktari wa nyanjani takriban 4,045 kuhamasisha jamii kuhusu chanjo pamoja na kuendeleza huduma hizo katika maeneo yaliyo na ugumu kufikiwa kutokana na kukosekana kwa vituo vya afya.
“Tukiwa lengo letu ni kufikia kila mwananchi ambaye anatakiwa kupata huduma ya chanjo, mikakati ambayo tumefanya ni kuimarisha na kugawa huduma za afya kupitia mfumo wa afya ya msingi afya mashinani. Nasema hivi kwasababu saa hii tuko na jopo la madaktari wa afya ya nyanjani 4,045 na kila daktari wa afya ya nyanjani ana nyumba 100 ama zaidi na tumeweka kila CHP ahakikishe watoto wote chini ya miaka miwili wamemaliza chanjo.” alisema Mumbo.
By Erickson Kadzeha