HabariMombasaNews

Mwashetani Aanza Rasmi Wadhifa wake kama mwenyekiti Mpya wa Bodi ya NTSA

Hatimaye Khatib Abdallah Mwashetani amechukua rasmi mamlaka kama mwenyekiti mpya asiye mtendaji wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama barabarani (NTSA).

Mbunge huyo wa zamani wa Lungalunga amewahakikishia Wakenya lengo na dhamira ya Mamlaka ya kushirikiana na wadau wote husika kuhakikisha huduma zinatolewa kwa ufanisi kwa mwananchi.

Akizungumza jijini Nairobi katika afisi kuu ya NTSA mnamo Jumatano Aprili 2 ambapo alichukua madaraka rasmi kufuatia uteuzi wake na Rais William Ruto wiki jana, Mwashetani aliwahakikishia Wakenya kuwa shirika hilo la usalama barabarani litafanya kile ambacho kiko ndani ya mamlaka yake ili kupunguza visa vya ajali barabarani.

Mwashetani ambaye pia aliwahi kuhudumu kama msaidizi wa Waziri wa Afya (CAS) kabla ya wadhfa huo kuvunjiliwa mbali, aidha amepongeza usimamizi wa NTSA na wafanyakazi kwa kazi nzuri ya kuhakikisha kuwa umma unahudumiwa vyema kote nchini.

Katika afisi hioz za NTSA wakati wa kukabidhiwa rasmi afisi yake, Mwashetani alipokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa NTSA George Njao na mkuu wa Huduma za Usaidizi wa Mashirika katika Mamlaka hiyo, Jacob Sisey.

Na Mjomba Rashid