HabariNewsSiasa

ODM Yapuuzilia mbali Madai ya Kalonzo na Wenzake ya Kuhujumu Uundwaji wa IEBC

Chama cha ODM Kimejitenga mbali na madai ya liyoibuliwa na viongozi wa upinzani kuwa chama hicho na kile cha UDA kinahujumu mchakato wa uteuzi wa IEBC.

Wakihutubia wanahabari baada ya mkutano uliohudhuriwa na kuongozwa na kinara wao Raila Odinga, Viongozi wa chama wamekana madai hayo yaliyoibuliwa na viongozi kadhaa wa Azimio na kuyataja kutokuwa na msingi wowote.

Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna amesema kuwa mchakato unaoendelea wa uteuzi wanachama kuunda upya Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC unatakelezwa kwa mujibu wa ripoti ya jopo la maridhiano la NADCO.

Tunazichukulia shutuma za baadhi ya viongozi wa Azimio kama jaribio la kudhalilisha jopo na matokeo ya mchakato mzima. Wakenya wamesubiri kwa muda mrefu kuwa na tume ya uchaguzi na hawatakabiliana na majaribio yoyote ya kuvuruga au kuchelewesha mchakato huo,” akasema Sifuna

Sifuna amesema kuwa kucheleweshwa kwa mchakato wa kuunda upya IEBC kulitokana na utata wa chama cha WIPER kushindwa kutatua mwakilishi wake katika jopo la uteuzi.

Inajulikana kuwa NADCO ilikuwa chini ya uenyekiti wa Kalonzo Musyoka, kiongozi wa Wiper. Wakenya wanafahamu fika kwamba kuchelewa sana kwa zoezi hili kulitokana na kushindwa kutatua uteuzi wa mwakilishi wa Wiper kwenye jopo la uteuzi. Wiper ilipata nafasi yake halali,” Sifuna aliongeza.

Kamati Kuu ya ODM, iliyokutana chini ya uenyekiti wa kinara wa chama hicho Raila Odinga, pia ilikariri kuwa chama hicho hakiko serikalini.

ODM haiko serikalini, na sijui ni mara ngapi tunapaswa kujibu swali hilo. Mtu anapotoa madai kama hayo, unapaswa kuuliza ni nini msingi wa madai hayo, kisha tunaweza kuhusika kutoka hapo,” alibainisha Sifuna.

Na Mjomba Rashid