Serikali inapania kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu iliyotangaza kuwa agizo linalowataka wazazi kulipa karo za shule kupitia mtandao wa eCitizen ni kinyume cha katiba.
Akithibitisha hatua hiyo Katibu Mkuu wa wizara ya elimu Julius Bitok amesema tayari wizara hiyo imeanza kuwasiliana na afisi ya mwanasheria mkuu ili kuanza mchakato hupo.
Bitok amelitetea agizo la kuelekeza ada kupitia jukwaa la e-Citizen akisema hatua hiyo ililenga uwazi katika kaunti za shule sawia na kuwalinda wazazi dhidi ya unynyasaji unaotekelezwa na baadhi ya wakuu wa shule.
“Tutatii mahakama. Lakini tutakata rufaa dhidi ya uamuzi huo kwa sababu eCitizen ni jukwaa ambalo liko wazi,” alisema Bitok.
Mnamo Januari 2024, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Elimu Belio Kipsang, kupitia waraka rasmi aliagiza malipo yote ya karo ya shule yafanywe kwenye jukwaa la eCitizen.
Hatahivyo Jaji Chacha Mwita, mnamo siku ya Jumanne alipiga marufuku utekelezwaji wa agizo agizo hilo, akilitaja kuwa kinyume cha sheria na kuwa hakukuwa na ushiriki wa umma kabla ya utekelezaji wake.
Pia alibainisha kuwa ada ya shilingi 50 inayotozwa kwa kufanikisha shughuli hiyo haina msingi wa kisheria.
Na Mohammed Mwajuba