Mamia ya familia katika kijiji cha Gasi eneobunge la Msambweni kaunti ya Kwale zimesalia bila makao baada ya nyumba zao kubomolewa chini ya ulinzi mkali wa polisi.
Wakaazi hao wamedai ubomozi huo ulitekelezwa mapema Jumatatu asubuhi Aprili 7, bila ilani yoyote na magenge ya vijana waliokuwa na mapanga na marungu.
Vijana hao waliojihami wanadaiwa kuharibu mali za wakazi hao huku maafisa wa usalama waliokuwepo wakitazama pasi kuingilia kati.
“Hatuwezi kuishi namna hii, leo hii watoto wetu wametawanyika na mvua hii tutakwenda wapi. Kwanza wametuvamia na kutbomolea bila notisi.”
Wamedai kuwa wamekuwa wakiishi katika eneo hilo kwa miaka mingi kama maskwota na kwamba tayari serikali ilikuwa imewatengea ekari 306, hivyo kuwepo njama za unyakuzi wa ardhi hiyo ambayo wamekuwa wakiishi kwa muda mrefu.
“Hii sehemu ilikuwa na lease na lease imeisha sasa wanataka kuinyakua wajinufaishe wapo na ndio maana wamelta askari saa kumi na moja asubuhi na hakuna hata notisi, mtu amelala anaamka nyumba inavunjwa hii ni haki?”
“Kwa nini sisi tudhulumiwe? Kwa sisi sio Wakenya na serikali ilitupa hii ardhi ya ekari 306 ili tufaidi sisi wakazi wa Gasi lakini sasa mbona haya?” akasema mkaazi mmoja.
Familia hizo zaidi ya 200 ambazo zitalazimika kulala nje na kupigwa na baridi ya usiku kucha zimelaani ubomozi huo sasa zikililia viongozi mbalimbali serikali ya kaunti ile ya kitaifa kuingilia kati ili wapate haki yao.
“Hatuwezi kuishi namna hii, hii ni dhulma ya kihistoria jhatuna viongozi kwani, hatuna Gavana hatuna seneta hatuna mbunge sisi tunafurushwa. Dhulma zilianza kitambo sana…
Sisi hapa hatutoki na tutakuwa hapa ni serikali iingilie kati itatua shida hii lakini hapa hatutoki.” Akasema mkaazi mmoja.
Huku hayo yakijiri, Wakaazi eneo la Chembe Kibambamche wadi ya Watamu eneo bunge la Kilifi Kaskazini wanalalamika kuhangaishwa na mabwenyenye wanaodai kumiliki kipande cha ardhi wanachoishi.
Wakiongozwa na Christine Samini Kazungu, wakaazi hao wameelezea kusikitishwa na hatua ya kunyanyaswa na mabwenyenye hao licha ya kuishi kwenye kipande hicho za ardhi kwa miaka zaidi ya 40 sasa.
“Tunawashangaa wamekuja wanasema watu waondoke, vipi wataondoka kwa kuhadaiwa na pesa chache? Tunaiomba serikali itunususru kutokana na dhuluma hii ili tupate haki yetu.’’ Mkaazi mmoja alizungumza kwa uchungu.
Aidha wakaazi hao wamemtaka kiongozi wa taifa kutimiza ahadi alizozitoa wakati wa ziara zake za maendeleo eneo la Pwani kuhusu matatizo ya ardhi Pwani ili wananchi waweze kuishi bila ya kuhangaishwa.
Wanawataka maafisa wa usalama eneo hilo kukoma kutumiwa na mabwenyenye ili kutimiza malengo yao huku wakiwahangaisha wakaazi.
“ Tunaishi maisha ya kuhangaika ni kama kwamba sisi si wakenya. Kwani wanataka tukaishi wapi kanma tunaambiwa tutoke huku?
Tafadhali tunakuomba rais wetu utimize ahadi yako na utuondoshee matatizo ya uskwota.” aliongeza mkaazi mwengine.
Na Waandishi Wetu