Wanafunzi zaidi ya 21,000 kwenye vyuo vya kiufundi takriban 483 humu nchini wanatarajiwa kufanya mtihani mwezi huu wa Aprili, mamlaka ya kitaifa ya kusimamia mafunzo ya kiufundi NITA, ikisema hii ni hatua moja wapo ya serikali ya kusaidia vijana kupata ajira kupitia ujuzi wanaopata kwenye vyuo hivyo vya kiufundi.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa mitihani hiyo katika chuo cha kiufundi cha Dzitsoni eneo bunge la Kilifi kusini, katibu wa wizara ya Leba Shadrack Mwadime amesema mitihani hiyo itawasaidia vijana katika kupata ajira ndani na nje ya nchi, akiongeza kuwa mamlaka ya kitaifa ya kusimamia mafunzo ya kiufundi NITA pia itatoa vyeti kwa wale walio na ujuzi japo hawajasomea vyuoni kazi wanazofanya.
“Zile ambazo tunaziita “trade tests” katika vituo 483 humu nchini na tuko na wanafunzi zaidi ya elfu 21 ambao watakuwa wanafanya mitihani hii. Kama mnavyofahamu mitihani hii ni “practical” asilimia 10 pekee ndio “theory” na katika misingi hiyo mwanafunzi anaweza kupewa cheti. Lakini kando na hivyo tunawahimiza vijana wetu ambao wamepata tajriba ya kazi tofauti tofauti huko nje na anahisi sasa anafaa kupata cheti NITA itakuja kumfanyia mtihani kisha wampe cheti.” alisema Mwadime.
Kwa upande wake mwenyekiti wa mamlaka ya kitaifa ya kusimamia mafunzo ya kiufundi NITA Aden Ali Nur amesema mamlaka hiyo huandaa mitihani mara tatu mwezi Aprili, Agosti na Desemba kila mwaka akiongeza kuwa mamlaka hiyo hutoa mafunzo kwa wanafunzi 150,000 kila mwaka na kuwa msimu huu wanatoa mafunzo ya aina 43 za ujuzi.
Aidha amebainisha kuwa vyeti vinavyotolewa na mamlaka hiyo hutoka nchini Uingereza na vinatambulika kimataifa.
“Kwa kawaida tunatoa mafunzo kwa wanafunzi laki moja na nusu kila mwaka katika aina tofauti tofauti za ujuzi. Na msimu huu tunatoa aina 43 za mafunzo. Kwanini tunafanya hivi? Kama alivyosema katibu kwamba kazi zipo huku nje ila vijana wetu wanakaa tu wakifikiria kuwa hakuna kazi na sasa kazi zinatoka kutoka kwa chuo kikuu mpaka kwa kuwa na ujuzi tu na hawa ndio watu kama wizara ya Leba tunawasafirisha ughaibuni kufanya kazi. Vyeti tunavyowapatia vinatoka nchini Uingereza na vinatambulika kimataifa.” alisema Nur
Mbunge wa Kilifi kusini aliyepia mwanakamati wa Leba katika bunge la kitaifa Ken Chonga ametoa wito kwa wazazi kuwahimiza vijana kujiunga na vyuo hivyo, na kutumia ujuzi wanaopata kustawisha maisha yao.
“Ni kuwe na imani kwamba inawezekana na tuwahimize wajiunge na vyuo hivi wasomee taaluma hizi na wale ambao wako na ujuzi wapate vyeti hivi. Na laziada ambalo kwamba tunaliangalia katika kutumia taasisi hii iwapo kwamba tutapata ile nafasi kwasababu tayari serikali imeanza kuweka saini za mikataba na mataifa mbali mbali. Nikupitia mpango kama huu ambapo tunaweza tukafungua vijana wetu na maisha yakageuka.” alisema Chonga.
Katibu wa wizara ya Leba Shadrack Mwadime vile vile ameeleza kuwa wizara hiyo inashirikiana na wadau mbali mbali kutoa hamasa mashinani kama njia ya kuhakikisha kuwa vijana hawalaghaiwi na mawakala bandia wanapotafuta ajira katika mataifa ya ughaibuni.
“Sisi kama wizara wakati huu tumeanza kuingia mashinani kwasababu vijana wengi wanatulaumu vile zile kazi za kwenda ng’ambo hawajui ni jinsi gani wanaweza kuzipata. Wengine wameangukia kwenye mikono ya wale wahalifu “rogue agencies” ambao wanaiba pesa zao na mwishowe hawawezi kuwapeleka huko ng’ambo kufanya kazi hizi. Wanawadanganya eti wanaenda na visitors visa waende wakafanye kazi haiwezekani! Kile ambacho unahitaji ni “work permit” na mwanzo wa kupata cheti hicho ni hapa Kenya. Kwa hivyo tunafanya kazi NITA, pamoja na Mamlaka ya kitaifa ya uajiri tukiingia mashinani ili tuweze kuwaeleza watoto wetu ni jinsi gani wanaweza kupata kazi hizi kwasababu kazi hizi zipo.” alisema Mwadime.
Ikumbukwe kufikia sasa ni vijana 7,000 pekee waliojiunga na vyuo vya kiufundi kaunti ya Kilifi ikilinganishwa na 40,000 idadi inayolengwa na serikali ya kaunti hiyo.
Erickson Kadzeha