Wizara ya Ulinzi imefichua kuwa ajali mbaya ya helkopta ya kijeshi iliyotokea Aprili 18, 2024, ambapo aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Francis Ogolla alifariki, ilisababishwa na hitilafu ya injini.
Ajali hiyo ya ndege ya ki jeshi iliyotokea eneo la Sendar kaunti ya Elgeyo Marakwet ilimwua Jenerali Ogolla na watu wengine 9.
Katika taarifa yake Ijumaa, Wizara hiyo imebaini kuwa ripoti ya uchunguzi iliyofanywa na Idara ya jeshi kuhusiana na ajali hiyo helikopta ya Bell Huey KAF 1501 ilipasuka kwa kishindo kikuu, ripoti ambayo ni sawa na ripoti za mashahidi walioshuhudia mlipuko mkubwa kwenye sehemu ya injini.
Baadaye ndege hiyo ilipoteza uwezo na nguvu kamili ya nishati, ambayo ilifuatiwa na kushuka kwa injini ya Revolutions Per Minute (RPM) na mabadiliko ya kelele ya injini.
Kuhusiana na ati ati na uvumi wa utepetevu ripoti hiyo imeeleza kuwa Wizara ya Ulinzi ilikagua misheni nzima tangu kuondoka kwa timu hiyo kutoka Uwanja wa Ndege wa Wilson hadi Kainuk, Chesogon, kabla ya kuelekea Shule ya Mafunzo ya Kuajiri Wanajeshi huko Eldoret, na ikabaini kuwa wafanyakazi hao walikuwa wamefanya ukaguzi wa ndege uliohitajika kabla ya kuanza safari.
Zaidi ya hayo, serikali imeondoa shaka na kupuuzilia mbali dhana ya hali mbaya ya hewa, ukosefu wa tajriba na ushirikiano wa wafanyakazi na uzoefu wa marubani kama sababu ambazo zingepelekea ajali hiyo, ikisisitiza kuwa marubani wote wawili walikuwa tayari kwa misheni hiyo kama ilivyoainishwa katika Taratibu za Kawaida za Uendeshaji kwenye Kitabu cha Maagizo ya Kuendesha Ndege Flying Order-(FOB).
Wakati wa kupanga misheni hiyo, serikali ilifichua kwamba wafanyakazi walikuwa na muda wa kutosha wa kufanya Ukaguzi wa Kabla ya Ndege kupaa na Wafanyakazi wa Kwanza na kwamba ndege hiyo pia ilifanyiwa huduma za ukaguzi kwa saa 25 kuanzia Aprili 2 hadi Aprili 5 2024, ili kuzingatia viwango vya juu zaidi vya usalama wa ndege.
Watu wengine waliofariki katika ajali hii ni pamoja na Brigedia Swaleh Said, aliyekuwa Kanali Duncan Keitanyi, Lutein Kanali David Sawe, Meja George Benson Magundu, Captain Sora Mohamed, Captain Hillary Litali, Sergent Mwandamizi John Kinyua Muriithi, Sergent Clinfons Omondi na Sergent Ruth Nyawira.
By Mjomba Rashid