HabariNews

Serikali yafutilia mbali leseni 500 za mawakala walaghai

Visa vya wananchi kulaghaiwa na mawakala bandia wanapotafuta ajira nje ya nchi vikiongezeka serikali imesema kuwa imeweka mikakati ya kupambana na ulaghai huo kwa kuwapokonywa leseni na kuwafungia nje mawakala watakao gundulika kuendeleza visa hivyo na hawatoruhusiwa tena kushiriki kwenye shughuli hiyo humu nchini.

Maelfu ya Wakenya wanaotafuta ajira mataifa ya ughaibuni wakiendelea kupoteza pesa zao kwa kuangukia katika mikono ya mawakala walaghai, onyo kali imetolewa kwa mawakala wanaojihusisha na visa hivyo kuwa hatua kali za sheria zitachukuliwa dhidi yao.

Kwa mujibu wa katibu wa wizara ya Leba Shadrack Mwadime, tayari serikali imefutilia mbali leseni 500 za mawakala walaghai na kuwapiga marufuku ya kushiriki shughuli hizo humu nchini huku uchunguzi zaidi ukiendelezwa kwa mawakala wengine wanaotajwa kwenye kashfa za ulaghai.

Ametoa wito kwa wananchi kupiga ripoti ili hatua za sheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya mawakala hao wanaoendelea kunufaika kwa njia zisizo halali.

Kama mnavyojua tumefutilia mbali leseni 500 za mawakala walaghai na tunaendelea kufutilia mbali leseni zaidi. Tunashirikiana kwa ukaribu sana na asasi za usalama na tutawatoa wote. Wananchi wakituletea malalamishi tu basi tunawatoa kutoka kwa sajili yetu. Mwananchi unapokosa kupiga ripoti nap engine pesa zako zimechukuliwa labda laki nne ama tano, mkenya anaweza kutoa pesa hizo wapi? Umehangaika kupata hizo pesa kwa hivyo itakuwa ni haki kwa hawa wahalifu wawekwe ndani kwasababu ni vitendo vya uhalifu wanavyofanya.” alisema Mwadime.

Ameongeza kuwa wakurugenzi wa kampuni za uwakala watalazimika kufika mbele ya kamati ya usaili kufanyiwa usaili kabla ya kupewa leseni ya kuendeleza shughuli hizo za uwakala.

“Kuhusu jambo hilo, kitu tunachosisitiza ni kuwa wakurugenzi wa kampuni za uwakala lazima wafike mbele ya kamati ya usaili, ili tujue ikiwa wewe ni miongoni mwa wale mawakala tuliowatoa kwenye sajili yetu kwasababu ya ulaghai basi usiweze kupata nafasi nyingine ya kudhulumu wakenya.” alisema Mwadime.

Katika kisa cha hivi karibuni mamia ya wakenya jijini Nairobi walilaghaiwa na mawakala kuwa wangetafutiwa ajira nchini Mauritius.

Erickson Kadzeha