Mashindano ya kitaifa ya chipukizi ya M-Pesa Jr NBA hatimaye yamefikia tamati baada ya fainali za kusisimua kurindima katika shule ya Agakhan mjini Mombasa.
Fainali hizo zilijumuisha timu 16 ( 8 wasichana na 8 wavulana)zilizotwaa ubingwa kwenye mashindano ya mkoa yaliyochezwa katika maeno ya Nairobi, Mombasa, Eldoret, Kisumu.
Shule ya msingi ya Olympic Jss kutoka Nairobi iliibuka kidedea katika fainali ya wasichana kwa kuwalaza Shelter academy ya Kisumu kwa vikapu 19-15.
Nao St. Johns Korogocho wa kuko huko Nairobi walitwaa ushindi kwenye upande wa wavulana baada ya kuwanyuka wenyeji wao Aghakhan academy kwa vikapu 30-23 na kuupaka matope msemo kuwa mcheza kwao hutuzwa.

Akizungumza na wanahabari baada ya mashindano hayo Michael Finley, Mwakilishi Mkuu nchini Kenya wa Shirikisho la mpira wa Vikapu Barani Afrika, NBA Africa, amesisitiza nia ya shirikisho hilo ya kukuza vipaji katika mchezo wa vikapu na kutoa mafunzo kwa makocha na chipukizi zaidi hasa kutoka maeneo ya mashinani.
“Tunalenga kupanua mashindano haya ili tufikie maeneo yote nchini na vilevile kutoa mafunzo kwa makocha zaidi kwani mchango wao ni mkubwa sana katika ukuaji wa mchezo huu.Pia tunapania kuwezesha wanafunzi kwa vifaa ikiwemo mipira,vikapu na viwanja ili waendele kucheza kwa urahisi sawia na kuboresha hadhi ya mchezo wa vikapu nchini Kenya.
Tuwe tayari kwa mashindano yajayo ambayo tunatazamia yatakuwa makubwa zaidi na kujumuisha wachezaji wengi chipukizi.” Alisema Micheal Finley.
Wachezaji Moses Ochieng wa St Johns Korogocho na Brenda Akinyi wa Olympic jss walitawazwa wachezaji bora wa mashindano hayo nao makocha wao Brian Lusaga wa St Johns na Ezra Alenga wa Olympic Jss wakachaguliwa kuwa makocha bora.
Kocha Ezra Alenga alikuwa na haya ya kusema baada ya timu yake kunyakua ubingwa:
“Tunawashukuru sana M-Pesa na Jr.NBA kwa mchango wao katika mchezo wa vikapu kwa wanafuzi wa shule za msingi kwani hapo awali mashindano katika mchezo huu yalikuwa yakianza ia kwenye ngazi ya shule za upili.
Haya yalikuwa Makala ya kwanza ya mashindano ya kitaifa ya vikapu M-PESA Jr. NBA kwa wachezaji wasiozidi miaka 16 yaliyoandaliwa kwa hisani ya M-pesa kwa ushirikiano na NBA na yalishirikisha zaidi ya wavulana na wasichana 10,000 kutoka maeneo manne nchini.
Mnamo Jumatatu, Aprili 7 wanafunzi bora 100 (50 wavulana na 50 wasichana) katika mashindano hayo walipewa mafunzo kuhusu mchezo wa vikapu kupitia mazoezi na hata vikao vya mafunzo au kliniki za mafunzo.
Fauka ya hayo wanafunzi hao walishiriki semina za mafunzo ya maisha na kupewa ujuzi wa kifedha,jinsi ya kutumia,kuhifadhi na hata kuwekeza fedha zao kupitia jukwaa la M-PESA Go.
By Mohammed Mwajuba