HabariNews

Rais Ruto Amsimamisha Kazi Mwenyekiti wa Taasisi ya BioVax kwa Uhusiano wake na Hospitali ya Mediheal

Rais William Ruto amemsimamisha kazi aliyekuwa Mbunge wa Kesses Dkt. Swarup Mishra kama Mwenyekiti wa Taasisi ya Kenya BioVax.

Haya yanajiri huku Hospitali ya Mediheal, ambayo ilianzishwa na Dkt. Mishra, ikichunguzwa kwa madai ya kuhusika na utovu wa nidhamu na ukiukaji wa maadili katika huduma za upandikizaji figo.

Katika taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Msemaji wa Ikulu Hussein Mohammed, Rais Ruto amechukua uamuzi wa kumsimamisha kazi Dkt. Mishra kama Mkurugenzi wa Taasisi ya Kenya BioVax ambaye pia ni mwanzilishi wa Hospitali hiyo ya Mediheal, na agizo hilo linaanza kutekelezwa mara moja na litaendelea kutumika hadi uchunguzi utakapokamilika.

“Kusimamishwa kutaendelea kutekelezwa ikisubiri matokeo ya uchunguzi kuhusu madai makubwa ya shughuli zisizo za kimaadili na haramu zinazohusisha taratibu za upandikizaji wa figo katika Hospitali ya Mediheal na Kituo cha Rutuba mjini Eldoret. Hospitali hiyo ilianzishwa na Dkt Mishra.” Ilisema Taarifa.

Hussein ameongeza Rais anasisitiza lengo la Serikali ya kupambana na rushwa, ikiwa ni pamoja na kudumisha uadilifu katika huduma za afya, usalama wa umma na haki kwa waathiriwa.

Uchunguzi ulioongozwa na serikali katika Hospitali ya Mediheal mjini Eldoret uligundua mapungufu makubwa katika mpango wa upandikizaji wa figo katika kituo hicho, na kuibua wasiwasi kuhusu uwezekano wa ulanguzi wa viungo vya mwili unaohusisha raia wa kigeni.

Haya yalijiri baada ya ujumbe wa kina wa kutafuta ukweli na timu ya taaluma mbalimbali iliyoteuliwa na Wizara ya Afya, kufuatia tahadhari kutoka kwa Jumuiya ya Kimataifa ya Upandikizaji.

Kwa sasa hospitali hiyo inachunguzwa kwa madai ya kuvuna figo kutoka kwa Wakenya maskini ambao wanaripotiwa kulipwa shilingi 294,000 na kisha kuziuza kwa wapokeaji katika mataifa ya kigeni kwa hadi shilingi milioni 3.2 kila moja.

By Mjomba Rashid