Rais William Ruto amewataka Maseneta na Wabunge kumpa idhini ya kusimamia ugavi wa fedha wa Hazina ya Ushuru wa Urekebishaji Barabara – Road Maintenance Levy Fund (RMLF).
Akizungumza wakati wa ibada ya Jumapili katika Kaunti ya Narok, Rais Ruto amesema kuwa wabunge wanapaswa kusitisha malumbano na mgogoro unaoendelea kuhusu udhibiti wa hazina hiyo na kumruhusu aongoze usambazaji wake.
Rais amesisitiza kuwa kuna haja kubwa ya kujenga barabara nchini kote na fedha alizo anazo katika afisi serikalini zitaruhusu utolewaji na uangalizi kwa urahisi, akifichua kuwa kufikia sasa serikali imelipa takriban shilingi bilioni 60 kukamilisha ujenzi wa barabara ambazo zilikuwa zimekwama.
Kulingana na rais fedha za hazina hiyo hazijatumiwa ifaavyo na iwapo ataachiwa usimamizi wa ugavi wa Hazina hiyo ataweza kushughulikia ujenzi wa barabara nyingi zaidi na kuwafaidi Wakenya.
“Mkiniwachia naweza kupanga pesa nyingi ya kutengeza hizi barabara zote kwa sababu pesa mnayochokua mnajenga sehemu kidogo tu halafu inaharibiwa na mvua, hivyo nawaomba waheshimiwa, na sio kwa lazima nasema naomba mkubali, mniruhusu nipange fedha hizo kwa namna zinavyoweza kuwanufaisha Wakenya zaidi ya jinsi zinavyotumika kwa sasa,” akasema Ruto.
Haya yanajiri huku Maseneta wakiungana na magavana katika vita vya kudhibiti Hazina hiyo ya RMLF ya shilingi bilioni 10.5, wakiwataka Wabunge kuacha azma yao ya kuinyemelea hazina hiyo.
Itakumbukuwa kuwa Wajumbe wa Kamati ya Fedha ya Seneti walisema hawataunga mkono mapendekezo yoyote katika Mswada wa Ugavi wa Ziada wa Serikali za Kaunti, mwaka 2025, ulio mbele ya Bunge kwa sasa, bila Hazina hiyo ya RMLF.
Kwa upande wao wabunge wakiongozwa na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah walisema wanalinda hazina hiyo RMLF ya dhidi ya kuporwa na magavana.
“Kama Bunge, tutashughulikia Mswada wa ziada wa mapato ya kaunti bila RMLF na wacha niwaambie, hautapitishwa katika Bunge hili. RMLF ni sawa waya wa umeme moja kwa moja katika Bunge hili ambao hutawahi kuugusa,” Ichung’wah alisema.
Wakati huo huo, Maseneta wamewaambia wabunge kutofuatilia udhibiti wa hazina hiyo.
Seneta wa Kakamega Boni Khalwale alisema pesa hizo zinafaa kudhibitiwa na magavana akisema wabunge wanataka tu kwa minajili ya ufisadi.
Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Ahmed Abdullahi alisema suala hilo liko mahakamani, akielezea imani kwamba matokeo ya uamuzi utakaotolewa yatakuwa kwa manufaa yao.
By Mjomba Rashid