HabariNews

Kina mama wachanga kufufua na kunufaika na talanta za michezo Kilifi

Kina mama wachanga zaidi ya 200 katika wadi ya Mnarani wamepata matumaini mapya ya kuendeleza talanta zao za michezo na kupata fursa kujiimarisha kimaisha kupitia ujuzi wa kiufundi watakaopewa pindi watakapo kuwa wakiendelea kushiriki mashindano ya michezo yaliyozinduliwa rasmi mapema leo katika chuo cha kiufundi cha Mkwajuni.

Kina mama hao wachanga zaidi ya 200 waliochini ya umri wa miaka 20 wanatarajiwa kupata nafasi ya pili ya kuendeleza talanta zao kupitia michezo hali inayotarajiwa kuwajumuisha kwenye jamii baada ya kuonekana kutelekezwa kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa mwakilishi wadi wa Mnarani Juma Chengo mashindano hayo yanalenga kufufua vipaji vya michezo kwa kina mama wachanga lakini pia kutoa nafasi za ajira kutokana na mafunzo ya ujuzi watakaopata kipindi wanashiriki mashindano hayo.

“Nimeona niweze kujitosa na kuandaa mashindano haya kwa kina mama wachanga ni watu ambao wametelekezwa na wao wenyewe ni kana kwamba wamekosa matumaini wakifikiria kwamba kuzaa ni mwisho wa maisha na pia ni mwisho wa talanta, lakini hiyo si kweli. Ndio maana tunajitahidi kuhakikisha kuwa kina mama wote wachanga eneo hili tunawaleta kwa mambo ya michezo na pia kuwapa mafunzo ya kuhusu ujuzi wanaoweza kutumia kujipatia ajira na waweze kujitegemea.” alisema Chengo.

Ameongeza kuwa kupitia michezo kina mama hao wachanga watapata fursa ya kuonekana na maajenti wa vilabu vikubwa ambapo wakifanikiwa kusajiliwa wataweza kubadilisha hali zao za kimaisha na pia za familia zao.

“Sasa tukiwapa mazingira mazuri ya kufufua talanta zao, wataonekana na vilabu vikubwa vitawanyakuwa na wataweza kujikimu kimaisha na pia kusaidia familia zao kama wachezaji wengine ambao wamefanikiwa kimaisha kupitia michezo ndio sababu swala hili tumelivalia njuga tuhakikishe kuwa wanafanakiwa kupitia spoti.” alisema Chengo.

Kwa upande wake waziri wa elimu, teknolojia na ubunifu kaunti ya Kilifi Felkin Kaingu ameeleza kuwa kunavyo vipaji vingi vya michezo kaunti ya Kilifi ila changamoto ni kuweka mazingira bora ya kukuza talanta hizo.

Aidha ameweka wazi kuwa serikali ya kaunti itatenga fedha kwenye bajeti ya mwaka ujao wa kifedha ili kuhakikisha kuwa vijana wenye talanta wanatafutiwa soko kimataifa.

“Kusema kweli katika dunia kuna vijana wengi wamefaulu kupitia michezo. Kwa hivyo tutahakikisha kuwa vijana wetu tunawapatia mazingira sahihi kukuza talanta zao na kujiendeleza kimaisha. Ile bajeti ambayo tuko nayo tutahakikisha kuwa tumeweka fedha za kutosha kuwapeleka vijana nchi za nje kufanyiwa majaribio na kuwatafutia soko katika vilabu vikubwa vya kimataifa.

“ Talanta tuko nazo hapa na haya mambo ya kusema watu wa Kilifi hawawezi kushiriki riadha kwasababu maswala ya riadha tunawawachia ndugu zetu kutoka bonde la ufa huo ni uongo, kandanda sio ndugu zetu kutoka magharibi na nyanza pekee wanaoweza kusakata kabumbu hata sisi pia tuwakali ila tatizo ni kuwa hatujawekeza katika kuweka mazingira bora ya kukuza talanta hizi.” alisema Kaingu.

Ikumbukwe hatua hii inawiana na ile ya taifa la Afrika kusini ya kuanzisha kandanda ya kina nyanya miaka miwili iliyopita ambao wamefanikiwa kucheza mechi kadhaa za kirafiki za kimataifa, ikiwa mechi yao ya punde kabisa walipata ushindi kwa kuwalaza kina nyanya kutoka nchini Kenya.

Erickson Kadzeha