Huku ziara ya Rais William Ruto nchini China ikiendelea, Taifa la Kenya limevuna pakubwa kupitia makubaliano ya kimaendeleo na kidiplomasia na taifa hilo la bara Asia.
Rais William Ruto na mwenyeji wake rais Xi Jinping wameshuhudia utiaji sahihi wa mikataba 24 ya makubaliano ikiwa ni njia mojawapo ya kuimarisha sekta mablimbali ikiwemo elimu, viwanda, uchumi wa majini, uvumbuzi wa kidijitali, teknolojia na usafiri.
Miongoni mwa mikataba hiyo ni pamoja na ushirikiano katika uvuvi na masuala ya baharini unaowiana na makubaliano ya ruzuku ya Shirika la Biashara Duniani (WTO).
Hatua hii inapania kuwezesha jamii za Pwani kukuza usimamazi endelevu wa rasilimali za baharini, kuzalisha nafasi za kazi sawia na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Vile vile ziara hiyo imezalisha ushirikiano katika nyanja za sayansi, teknolojia na uvumbuzi mataifa hayo yakitarajiwa kufanya kazi kwa ukaribu kwenye utafiti jambo ambalo litawezesha wanasayansi, wajasiriamali na watafiti nchini kufikia utaalamu wa hali ya juu.
By Mohammed Mwajuba