Wakazi wa kaunti ya Tana River wanaoishi maeneo ya pembezoni mwa mto Tana wametakiwa kuchukua tahadhari kuhusu ongezeko la viwango vya maji katika mto huo.
Shirika la Msalaba Mwekundu limesema kwamba huenda maeneo ya nyanda za chini ya mto Tana yakasombwa na mafuriko kutokana na mvua kaubwa inayoshuhudiwa katika nyanda za juu.
Sasa limewarai wakaazi wajihadhari licha ya idara ya utabiri wa hali ya hewa (MET) kutangaza kushuhudiwa kwa mvua chache katika eneo hilo.
Abubakar Roba ni msimamizi wa shirika la Msalaba Mwekundu kaunti ya Tana River na ameeleza kuwa huenda mvua zikaongezeka zaidi katika nyanda za juu na huenda maafa yakawa makubwa.
Amedokeza kuwa tayari viwango vya maji katika Mto Tana vimeongezeka na hivyo kuwepo haja ya wakazi kuchukua tahadhari ya mapema.
“Mvua itakuwa nyingi zaidi kwa nyanda za juu na inamanaisha tutapata mafuriko. Ile hali tuko nayo kiwango ya maji imeanza kuongezeka kwa kiasi kikubwa sana kwa siku mbili zilizopita maji kutoka Garissa na inaashiria kuwa kadri inavyoongezeka na maji kupitia kuja sehemu za chini maafa yake yanaweza kuwa mengi zaidi.” Akasema.
Na Mwandishi Wetu