HabariNews

Vijana waaswa kutumia mitandao kujipatia ajira badala ya burudani.

Wito umetolewa kwa vijana kutumia mitandao kujitafutia ajira badala ya kutumia muda mwingi kwenye mitandao hiyo kwa maswala ya burudani. Ikielezwa kuwa kunazo nafasi nyingi za kujiimarisha kimaisha kujipatia ajira mitandaoni.

Tatizo la ukosefu wa ajira likiendelea kuwakabili wengi, vijana wamehimizwa kukumbatia nafasi za ajira zinazotokea mitandaoni kujistawisha kiuchumi.

Kwa mujibu wa mkurugenzi ukanda wa pwani wa kampuni ya AI ANIMAL HUSBANDRY LIMITED Victor Opiyo, inayojihusisha na ufugaji wa mitandaoni, zaidi ya Wakenya 350,000 wamejisajili kwenye kampuni hiyo ya mtandaoni tangu kuanzishwa kwake humu nchini miezi 10 iliyopita na wanaendelea kufaidika, wengine wakipata takriban shilingi 15,000 kwa siku.

Kampuni hiyo inalenga kupata usajili wa watu milioni moja watakaoendelea kushiriki uwekezaji wa ufugaji wa mitandaoni.

Vijana wengi wanajishughulisha sana na mambo ya burudani kwenye mitandao lakini tumekuja kugundua wakipata mtandao unaowapatia ajira kama huu wa AI ANIMAL HUSBANDRY LIMITED vijana hawa kwa muda mfupi tu akichukua simu yake ya rununu inaweza kuunganisha mtandao anaweza kubonyeza na kutumia hiyo nafasi kujistawisha kiuchumi.” alisema Opiyo.

Ignetius Wanyonyi mmoja wa wafugaji wanaowekeza mitandaoni anasema mradi huo unalenga kuwainua kiuchumi wakazi wa tabaka la chini, kwani mtaji unaohitajika kushiriki ufugaji huo ni mdogo.

“Kushikiriki kuwa mfugaji kunahitaji mambo machache sana. Kwanza lazima uwe umetimiza umri wa miaka 18, uwe na kitambulisho cha kitaifa, uwe Mkenya, na uwe na simu inayoweza kukuunganisha kwenye mtandao. Kisha unafaa kuwa na ule mtaji ambao utanunulia ule mfugo unaotaka, na ule mdogo kabisa ni shilingi 1,000 na ule mfugo ghali zaidi ni shilingi 100,000 kwa hivyo inakidhi mahitaji ya kila tabaka la Wakenya na kutokana na hali ngumu za kiuchumi mradi kama huu unakuja kuwasaidia Wakenya wengi.” alisema Wanyonyi.

Merceline Onong’a anasema amejiunga na uwekezaji huo wa ufugaji mitandaoni baada ya kumaliza masomo yake chuo kikuu na kupata shahada ya usimamizi wa miradi ila kwa kipindi kirefu hajafanikiwa kupata ajira.

“Tayari mimi ni mfugaji na kwa siku napata faida ya takriban shilingi 4,800 na nina mifugo kadhaa. Mpaka kufikia sasa nimetoa takriban shilingi 70,000 kwenye akaunti yangu na kuzitumia kwa mambo yangu binafsi.” alisema Onong’a.

Hellen Wanga muwekezaji mwengine wa ufugaji mitandaoni anasema kuwa mfumo huu wa uwekezaji ni tofauti na ule wa kamari.

“AI ANIMAL HUSBANDRY LIMITED ni uwekezaji mzuri ni tofauti na mchezo wa kamari ya pata potea, ni uwekezaji. Vile vile tunakuwa na mikutano ambapo tunafunzwa zaidi jinsi ya kuwekeza na kufanya ufugaji huu wa mitandaoni. Binafsi namaliza wiki yangu ya kwanza kesho tangu nimejisajili kwa hii kampuni na tayari nimepata faida ya shilingi 8,000. Unachohitajika kufanya ni kuhakikisha kuwa kila wakati unawalisha wale mifugo wako mtandaoni.” alisema Wanga.

Hata hivyo mkurugenzi wa ukanda wa pwani wa kampuni ya AI ANIMAL HUSBANDRL LIMITED Victor Opiyo amesisitiza kuwa swala la usalama mtandaoni limepewa kipaumbele ili kuepusha wanaoshiriki ufugaji huo wa mitandaoni kulaghaiwa.

“Mambo ya ulaghai yametambulika sana katika biashara ya mtandao hasa ajira mtandaoni. AI ANIMAL HUSBANDRY LIMITED imekuja na mikakati tofauti tofauti kuhakikisha kwamba mambo kama haya yanaweza kudhibitiwa. Tumezingatia pia zile nywila “password” ambazo tunaziweka pale wakati mfugaji anajisajili zinakuwa tofauti na zile za kutoa pesa, na zile zakuingia katika akaunti yake. Hizo zinakuwa zake binafsi na tunahakikisha kwamba anazidhibiti mwenyewe.” alisema Opiyo.

Hayo yamejiri wakati wa kikao kilichowaleta pamoja wakufugaji wa mitandaoni kote nchini kupitia kampuni ya AI ANIMAL HUSBANDRY LIMITED mjini Mombasa.

Erickson Kadzeha.