HabariLifestyleNewsSiasa

Atwoli ashinikiza Serikali Kuwapa Wafanyakazi Afueni ya Makato ya Ushuru

Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU) Francis Atwoli ameitaka serikali kurekebisha usanifu wa makato ya ushuru ili kuwapa afueni wafanyakazi wa Kenya.

Akizungumza wakati wa sherehe za Leba katika bustani ya Uhuru Gardens jijini Nairobi, Kiongozi huyo wa COTU amesema kuwa makato ya kila mwezi yanafaa tu kuathiri mishahara ya kimsingi ya wafanyakazi wa Kenya na wala sio malipo yao ya jumla.

Ametoa wito kwa Rais William Ruto kulivalia njuga na kuliangazia ombi lake hilo, akibainisha kuwa mishahara ya wafanyakazi nchini inaathiriwa pakubwa na makato hayo ya ushuru.

Atwoli amesema kuwa muda wa ziada wa kazi, posho au bonasi zisijumuishwe kwenye makato ya kila mwezi.

Makato yote ya mishahara na makato ya kisheria yanapaswa kuwa ya malipo ya msingi na si ya jumla ambapo mtu anaweza kuwa amefanya kazi ngumu kwa muda wa ziada na hatambui kitu,” akabainisha Atwoli.

Haya yanajiri huku Wakenya wakilalamikia ongezeko la mzigo wa ushuru uliowekwa na serikali ya Rais Ruto, baada ya kujumuisha maelfu ya makato ya ziada miongoni mwao, Ushuru wa Nyumba na Hazina ya Bima ya Afya ya Jamii (SHIF).

By Mjomba Rashid