Rais William Ruto ameendelea kutetea hatua na maamuzi anayoendelea kufanya akikariri kwamba hataogopa kuchukua njia ya uongozi isiyopendwa ili kuwaletea Wakenya maendeleo.
Akizungumza wakati wa sherehe za 60 za Siku ya Wafanyakazi (Leba Dei) katika bustani ya Uhuru jijini Nairobi, Rais Ruto amebainisha kwamba maamuzi yake yasiyopendeza yamechangia pakubwa taifa kufikia ukuaji wa kasi.
“Ninataka kuwaahidi watu wa Kenya kwamba nitafanya uamuzi sahihi kila wakati kuhakikisha kwamba Kenya inafanya maendeleo kwa sababu nina deni kwa Wakenya kufanya maamuzi sahihi,”
Wakati mwingine wanaweza wasiwe maarufu lakini ni maamuzi sahihi ambayo yatabadilisha hatima ya nchi yetu. Nina imani kubwa katika mustakabali wa nchi yetu.” Ruto alisema.
Ameshikilia kuwa tangu achukue mamlaka mwaka wa 2022, uongozi wake umeweza kuifanya Kenya kuwa ya 6 kwa uchumi mkubwa barani Afrika.
Utawala wa Rais Ruto umeangazia muundo wake wa maendeleo kwenye Ajenda ya Mabadiliko ya Kiuchumi ya kutoka chini kwenda Juu (Bottom-Up Economic Transformation Agenda) maarufu (BETA).
“Kuchochea ukuaji wa uchumi, kutoa ufanisi, kuongeza ushindani, na kupanua fursa. Kwa kweli, vifungu vyake vimeundwa ili kutoa unafuu unaolengwa kwa wafanyabiashara na wafanyikazi, na kuunga mkono ari ya biashara na tija,” Ruto akasema.
Wakati uo huo Rais amepigia debe mswada wa fedha mwaka 2025 ulioidhinishwa na baraza la Mawaziri na hatimaye kuwasilishwa katika bunge la kitaifa kujadiliwa.
Kulingana na rais Mswada wa fedha 2025 umeundwa kwa uangalifu ili kuchochea ukuaji wa uchumi, kutoa ufanisi na kuongeza uwezo na pia kupanua fursa mbalimbali za maendeleo katika sekta mbalimbali.
Rais amesema katika mswada huo utawataka waajiri kuwafanyia wepesi wafanyakazi wao kwa kuwaondolea uzito na makato ya mishahara wanayopokea wakati wa kukata makato yao ya kila mwezi ya PAYE.
“Hii itaongeza ufanisi na kuwanufaisha wafanyakazi mara moja,” alibainisha Rais.
By Mjomba Rashid