Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki amepuuzilia mbali viongozi wa upinzani anaodai kuchochea upinzani wa umma dhidi ya utawala wa Kenya Kwanza.
Wakati wa mkutano na viongozi wa Kaunti ya Nyandarua na wabunge katika makazi yake ya Karen, Kindiki amesisitiza uwajibikaji na umakini wa serikali katika kutimiza ahadi zake za kabla ya uchaguzi kinyume na ngonjera za kisiasa.
Kindiki amewaonya wakosoaji wa serikali kujiandaa kwa kile alichokiita ‘mapambano makali ya kisiasa’ katika uchaguzi mkuu wa 2027, akiwa na imani kwamba rekodi ya utawala itathibitisha mbivu na mbichi.
“Lengo letu linabaki kwenye huduma, sio kelele za kisiasa,” alisema.
Akiangazia maendeleo tangu aingie madarakani miezi sita iliyopita, Naibu huyo wa rais ametaja uthabiti wa uchumi, ikiwa ni pamoja na kuimarishwa kwa shilingi ya Kenya kama ushahidi wa athari za uwajibikaji wa serikali.
Zaidi ya hayo, amebainisha ujenzi unaoendelea wa masoko 400 ya kisasa kote nchini-ahadi kuu ya Kenya Kwanza inayolenga kuchochea uchumi wa hapa nchini.
Kindiki akikariri kujitolea kwake kuhakikisha ahadi za maendeleo za Rais William Ruto zinatekelezwa kwa usawa katika maeneo yote, huku akihimiza kuwa na subira wakati mageuzi yakishika kasi.
Huu ulikuwa mkutano wake wa pili wa mashauriano kufanyika katika makazi rasmi ya Naibu huyo wa rais huko Karen baada ya mapumziko mafupi.
Waliohudhuria ni pamoja na Faith Gitau (Mwakilishi wa Wanawake, kaunti ya Nyandarua), wabunge Kwenya Thuku wa (Kinangop), mbunge wa Ndaragwa George Gachagua, na Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah.
By Mjomba Rashid