Shughuli za masomo eneo la Midoina wadi ya Bamba eneobunge la Ganze zinakumbwa na ati ati na hofu ya kusambaratika kutokana na uvamizi wa mara kwa mara wa Ndovu.
Hali hii iliyotajwa kuweka hatarini maisha ya wakazi hasa wanafunzi wa shule za eneo hilo, huku wasijue hatma yao baada ya kusalia nyumbani kwa siku kadhaa sasa wakihofia usalama wao.
Kwa wanafunzi katika shule ya msingi Midoina wadi ya Bamba eneobunge hilo la Ganze walijikuta njia panda na kukosa kuhudhuria masomo kwa siku kadhaa sasa baada ya kundi la Ndovu kuvamia maeneo hayo hali iliyosababisha hofu ya usalama wao.
Kwa mujibu wa wazazi wa maeneo hayo ndovu hao wamekuwa wakiongezeka kila uchao na hivyo kuzua taharuki, hofu ya usalama wao na kuwalazimu kuwazuia watoto wao kuhudhuria masomo kwa kuhofia usalama wa watoto hasa nyakati za asubuhi na jioni ambapo ndovu hao huzura njiani na kuhatarisha maisha ya wanafunzi hao.
“Tumeathirika sana na ujio wa Ndovu hawa hali ambayo inakuwa ngumu kuruhusu watoto wetu kwenda shuleni kwa sababu usalama wa watoto wetu hakuna,serikali iko na uwezo mkubwa sana kuwafurusha hawa ndovu ili kuwaregesha kule kunakostahili sio kurandaranda mahali binadamu wanaishi.” Akasema mzazi mmoja.
Mwalimu Charo ni mmoja wa wazazi mwenye watoto watano na akasema haya: Niko na watoto 5 na wote hawajahudhuria masomo hali inayowarudisha nyuma kimasomo,sio hayo pekee tegemeo letu shambani limevamiwa na wanyamapori hawa na kukosa hata tumaini la chakula.”
Kwa upande wake mwenyekiti wa shule ya Upili ya Midoina Anderson Kazungu hatua hiyo haijaathiri shule ya msingi pekee bali pia ile ya upili, kwani licha ya shule hiyo kuwa na wanafunzi zaidi ya 100 waliohudhuria masomo hawafiki nusu ya wanafunzi hao.
“Kwa shule ya upili wanafunzi ambao hawajahudhuria masono ni kama asilimia 50 hivi na waliohudhuria ni wale wanaoishi maeneo ya karibu pekee, watafika vipi shuleni ikiwa ndovu wametapakaa kila mahali na wanafunzi hawawezi kurauka kufika shuleni? Akasema Kazungu.
Hatua hiyo ilijiri siku kadhaa baada ya mwakilishi wadi wa Bamba Said Mohammed Kadhengi kuahidi kuingilia kati suala hilo kwa kuwashinikiza wadau husika kuwajika.
“Tumepanga mikutano ya usalama wiki hii ambapo tutakuwa maeneo ya Goshi na Midoina tukishirikisha maafisa wa KWS pamoja jamii ili kuona tutasaidia vipi hali ilivyo kwa sasa,” akabaini Mohammed.
Kero la ndovu katika eneo hilo la Ganze limeendelea kuwa kikwazo kwa maisha ya kawaida ya wakazi, athari za uvamizi wa ndovu hao wanaotokea mbuga ya wanyama ya Tsavo Mashariki, zikidhihirika katika sekta ya elimu ambayo tayari imekuwa ikidorora na kuyumbishwa na athari za mawimbi Makali ya baa la njaa, ukame wa muda mrefu na mabadiliko ya tabianchi.
Ndovu hao sasa wakitishia kusambaratisha juhudi za wakazi walizowekeza katika elimu na kilimo kama tumaini lao la mwisho la kujiendelea.
NA SIMON CEPHAS.