Kina mama zaidi ya 100 wamewezeshwa kiuchumi kaunti ya Kilifi baada ya kupokezwa hundi ya shilingi milioni 1.8 kuendeleza miradi itakayowawezesha kujikimu kimaisha.
Kwa mujibu wa mshirikishi wa nyanjani kaunti ya Kilifi wa shirika la Islamic Relief Kenya Ahmed Osman Salat, kina mama zaidi ya 100 wanaopitia hali ngumu za kimaisha watanufaika kwa kiwango kikubwa kuinua jamii zao kiuchumi, kulipia matibabu pamoja na kuimarisha viwango vya kielimu kwa wanao kwani kina mama hao watakuwa na uwezo wa kuwalipia karo za shule.
Ameongeza kuwa licha ya kuwawezesha wanawake, mradi huo pia utasaidia kupunguza visa vya ukatili wa kijinsia ambao umekuwa ukishuhudiwa katika kaunti ya Kilifi.
“Ningeomba Islamic relief USA msaada huu usiwe wa mwisho, kwasababu huu ni msaada ambao unaweza kuimarisha jamii yetu na kuishi maisha mazuri. Hawa kina mama wako na familia zao na na wanapitia hali ngumu za kiuchumi wengi wanapata mlo mmoja pekee kwa siku. Naamini kupitia mradi huu karo za shule za watoto wao zitalipwa, matibabu hospitalini yatalipiwa na changamoto nyingine za kifamilia zitasulushika.” alisema Salat.
Naibu gavana wa Kilifi Florence Chibule Mbetsa amesema kuwawezesha kina mama kuna umuhimu mkubwa kwani huchangia maendeleo katika jamii huku ikizingatiwa kuwa asilimia 52 ya wakazi kaunti ya Kilifi ni wanawake. Aidha ametoa wito kwa mashirika mengine kujitokeza na kuanzisha miradi ambayo itasaidia kuimarisha jamii kiuchumi.
“Kitu ambacho kinamlenga mama ama mwanamke hakika ni kitu ambacho kitadumu. Manake nguzo inayobeba familia ni kina mama. Unapomuwezesha mama unaiwezesha jamii nzima. Takwimu za hapa kaunti ya Kilifi zinaonesha kuwa asilimia 52 ni wanawake, na hiyo asilimia 48 ni wanaume kwa hivyo tukiwashika hawa kina mama vizuri hawa kina mama watafika mbali.” alisema Mbetsa.
Wakiongozwa na Bibiana Salim na Gladys Neema Baya kina mama hao wanasema hundi za shilingi elfu 368 walizopokea zitaimarisha miradi yao pamoja na kujijenga kimaisha kwani wanategemewa na jamii zao.
“Sisi kina mama tunategemewa katika jamii zetu. Na sisi kina mama ndio ambao tunatowa mambo mengi ya matumizi ya majumbani mwetu. Uchumi ama radi ukiwa mdogo mambo yanasambaratika. Na ninatoa shukurani kubwa kwa shirika hili la Islamic Relief USA kwa kutupa msaada huu wa shilingi elfu 368,600.” alisema Bi. Salim
“Tulikuwa tunatamani siku kama ya leo ifike maana tukitaka kusongea vile sisi ni wazazi, mara mambo ya shule karo zinatakikana mara hakuna chakula basi tunarudi nyuma lakini sasa vile tulivypata hii hundi tuko na furaha sana maana tunajua mradi wetu tutauinua na watoto wetu watasoma.” alisema Bi. Baya.
Erickson Kadzeha.