Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewaonya wanaharakati ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki kuingia Tanzania na kutoa matamko yanayoweza kuchochea uvunjifu wa amani katika taifa hilo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa sera ya mambo ya nje, toleo la mwaka 2024, Rais Samia Suluhu Hassan ametumia jukwaa hilo kuwaonya wanaharakati ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki kuacha kuingia nchini na kutoa matamko yanayoweza kuvuruga amani ya nchi hiyo.
“Tumeanza kuona mtiririko au mwenendo wa wanaharakati wa region hii, kuanza kuingilia mambo yetu huku, sasa kama kwao wameshadhibitiwa wasije kwetu huku kutuharibia, tusitoe nafasi,” akasema rais Samia.
Rais Samia amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua za haraka kwa kutoa ufafanuzi, kukanusha au kurekebisha badala ya kuruhusu Tanzania kuwa shamba la bibi kwa kila mmoja kuingia na kutoa tamko lake.
“Walishaharibu kwao, walishavuruga kwao… nimeona clip kadhaa za kunisema niko na upendeleo niko bias, ninalofanya ni kulinda nchi yangu na ndio wajibu nilipewa.
Hatutatoa nafasi kwa kiumbe yoyote kuja kutuvurugia hapa awe yuko ndani awe anatoka nje hatutatoa hiyo nafasi.” Akasema rais Suluhu.
Itakumbukwa kwamba mnamo siku ya Jumapili mawakili pamoja na wanaharakati kutoka Kenya waliosafiri nchini Tanzania kusikiliza na kumwakilisha Tundu Lissu kwenye kesi yake ya uhaini walizuiwa uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere na kurejeshwa makwao.
Hii ni licha ya kwenda huko kwa ualishi rasmi wa Chama cha Mawakili wa Afrika Mashariki.
Hata hivyo aliyekuwa jaji mkuu nchini Kenya David Maraga amehudhuria vikao vya mahakama siku ya Jumatatu na kusikiliza kesi inayomkabili Tundu Lissu wa CHADEMA, kesi ambayo imeahirishwa hadi mwezi ujao Juni 2.
Hii ni baada ya upande wa Serikali kuiomba Mahakama muda zaidi wa siku 14 ili kukamilisha uchunguzi wake.
By Mjomba Rashid na Mashirika