HabariNews

Maelfu ya vijana wajitokeza kwa zoezi la kusaka ajira ughaibuni

Maelfu ya vijana kaunti ya Kilifi wamejitokeza katika zoezi la kusaka ajira ughaibuni mjini Vipingo eneo bunge la Kilifi kusini katika mpango wa serikali kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana.

Shughuli hiyo iliyoandaliwa kwa ushirikiano wa mbunge wa Kilifi kusini na mamlaka ya kitaifa ya ajira NEA, imeshuhudia vijana wakijitokeza kutoka kila pembe ya kaunti ya Kilifi, ikiwa ni dhihirisho kamili kuwa kuna changamoto ya ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana.

Kwa mujibu wa Ruth Mailu ofisa msimamizi wa huduma za ajira katika mamlaka ya kitaifa ya ajira NEA, shirika hilo limefanikiwa kupata waajiri kutoka nchini Dubai watakaowaunganisha na vijana hao huku akisisitiza kuwa mamlaka hiyo imeweka mikakati ya kuwafungia nje walaghai pamoja na mawakala ambao hawajasajiliwa rasmi kuendeleza shughuli za kutafutia wakazi ajira nje ya nchi.

“Tuko na mashirika ya uwakala wa kibinafsi nyanjani ambayo wanadhibitiwa na mamlaka ya kitaifa ya ajira NEA, yananafasi za ajira na yanafanya usajili wa wafanyakazi katika vitengo mbali mbali nchini Dubai. Jambo ambalo naweza kuwaambia wakenya ni kwamba zile kazi zilizohapa na zoezi la kuwasajili vijana katika kaunti tofauti tofauti linalofanywa kwa ushirikiano wa NEA na serikali si ulaghai. Mashirika yetu ya uwakala huwa yamepewa ithibati ya kuendeleza kazi hiyo baada ya kupigwa msasa, na yamesajiliwa rasmi na zile kazi zinazotolewa na mawakala hao ni za ukweli.” alisema Mailu.   

Victor Katana msaidizi wa mbunge wa Kilifi kusini na aliyepia mwenyekiti wa kamati ya leba katika bunge la kitaifa Ken Chonga anasema vijana zaidi ya elfu moja wamejitokeza kwenye shughuli hiyo ya kusaka ajira nje ya nchi, huku akidokeza kuwa wengi wa vijana hao wamesomea taaluma za utalii, hoteli, udereva na wengine wakiwa na taaluma za udaktari.

Ameongeza kuwa ofisi ya mbunge imeishirikisha mamlaka ya kitaifa ya ajira kwani ni kupitia mamlaka hiyo mawakala hufanyiwa uchunguzi kabla kuruhusiwa kuendeleza shughuli zozote za kutafutia wakenya ajira nje ya nchi.

Vijana zaidi ya 1012 wameweza kujitokeza kuja kutafuta ajira ughaibuni na kuona jinsi shughuli hii inavyofanyika. Vijana wengi waliojitokeza wamesomea taaluma za hoteli, udereva na wengine kama 200 wamesomea udaktari vile vile wamekuja kutafuta nafasi ya kwenda nje kufanya kazi.” alisema Katana.

Aidha vijana waliojitokeza katika zoezi hilo wameeleza matumaini yao ya kupata ajira nje ya nchi wakidai kuwa ni njia ambayo itawasaidia kujijenga kimaisha ikizingatiwa kuwa wengi wao wanapitia hali ngumu za kiuchumi. Kennedy Baraka, Felister Ali na Stephen Vugo ni baadhi ya vijana waliojitokeza kwenye zoezi hilo.

Kenya ni kugumu maisha sio rahisi. Kwa mtu kama mimi ninaposkia taarifa hizo na vile niko na cheti changu cha kusafiria huwa najitokeza mara moja hata kama nafanya kazi za sulubu kujikimu kimaisha.” alisema Baraka.

Zoezi limekuwa sawa, twangojea majibu yao vile yatakavyokuwa. Hakuna ufisadi wowote katika zoezi hili. Kabla nije hapa nimekuwa nikifanya kazi za humu humu mitaani tu. Mbunge wetu anajali watu wake ameona jinsi tunavyoteseka ndiposa ameleta mradi kama huu vijana tuweze kusaidika.” alisema Bi. Ali.

Mimi matarajio yangu ni kwamba Mungu anisaidie niwe nimepita hayo mahojiano japo kuwa mwenyewe najiamini na niweze kuwa mmoja wao wa wale ambao watasafiri kwenda nje ya nchi kufanya kazi. Zoezi limekuwa sawa na huru na nilikuwa natafuta nafasi kuwa dereva nchi za ughaibuni.” alisema Vugo.

Erickson Kadzeha.