HabariNews

Boniface Mwangi Aachiliwa Huru; Asafirishwa kwa barabara na kuachwa Ukunda, Kwale

Mwanaharakati wa Kenya Boniface Mwangi ameachiliwa kutoka kizuizini baada ya kuzuiliwa kwa muda wa siku tatu na mamlaka ya Tanzania.

Imearifiwa kuwa Mwangi amesafirishwa kutoka Tanzania kupitia usafiri wa barabarani, na kuachiliwa mjini Ukunda kaunti ya Kwale; ambapo kwa mujibu wa familia yake alikimbizwa hospitalini kwa uchunguzi wa kiafya.

Mkurugenzi Mtendaji wa Vocal Africa Hussein Khalid amewaambia wanahabari kwamba Mwangi kwa sasa yuko Mombasa na anatazamiwa kuabiri ndege hadi Nairobi.

Mwangi alikamatwa na watu wanaoshukiwa kuwa maafisa wa kijeshi baada ya kusafiri kutazama kesi ya uhaini ya kiongozi wa upinzani Tanzania Tundu Lissu siku ya Jumatatu.

Mwangi alikuwa miongoni mwa wanaharakati na wanasheria kadhaa wa Afrika Mashariki waliosafiri hadi Tanzania kusimama katika mshikamano na Lissu.

Wengi wao, hata hivyo walikataliwa kuingia baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam siku ya Jumapili na Jumatatu, wakazuiliwa kisha wakafukuzwa Nairobi.

Kukamatwa kwake Boniface kulizua mjadala na tandabelua kutoka kwa serikali huku Wizara ya Mambo ya Nje nchini ikisema mamlaka ya Tanzania imewanyima fursa ya kumfikia Mwangi.

Katika taarifa yake awali, wizara hiyo ilisema ‘licha ya maombi kadhaa,’ maafisa wa Serikali ya Kenya wamenyimwa ufikiaji wa kibalozi na kupata habari kuhusu Boniface Mwangi.

Itakumbukwa kuwa mnamo siku ya Jumatatu, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika hotuba yake alibaini kwamba wanaharakati wa kigeni hawataruhusiwa “kuingilia” masuala ya ndani ya Tanzania.

By Mjomba Rashid