Wakili tajika na Kiongozi wa chama cha PLP Martha Karua ameyaandikia barua mashirika mbalimbali barani Afrika kushinikizwa utawala wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu uchukuliwe hatua za haraka.
Hii ni kufuatia kuwekwa kizuizini na kuteswa kwa wanaharakati wa haki za binadamu Boniface Mwangi wa hapa nchini na mwenzake Agather Atuhaire wa Uganda.
Katika barua iliyotumwa kwa Umoja wa Afrika (AU), Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Sekretarieti ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Karua ameeleza kuwa kuwaweka kizuizini wawili hao kulikiuka viwango vya kimataifa vya haki za binadamu na kuweka historia mbaya ya maadili ya kidemokrasia katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa Karua, wanaharakati hao walikuwa sehemu ya ujumbe wa waangalizi wa Afrika Mashariki nchini Tanzania kufuatilia kesi ya uhaini inayomkabili kiongozi wa upinzani Tundu Lissu, lakini walipofika walikamatwa na kuzuiliwa na mamlaka.
“Kuzuiliwa kwa Mwangi na Atuhire kulitanguliwa na kufukuzwa nchini kwa Waangalizi wengine sita wa Mahakama ya Kimataifa ambao ni pamoja na Jaji Mkuu wa zamani, Waziri wa zamani wa Sheria na Mjumbe wa Baraza la Wanasheria wa Kenya ambao walikuwa wamefika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa misheni hiyo hiyo,” Karua alieleza.
Karua ameorodhesha matakwa kumi kwa mashirika ya bara Afrika na washirika wa kimataifa kupunguza suala hilo, akitaka mashirika hayo kutoa hati rasmi za kidiplomasia kwa serikali ya Tanzania kuomba ufafanuzi kuhusu mahali alipo Atuhaire.
Matakwa mengine ni pamoja na kuanzisha taratibu zao za ufuatiliaji wa haki za binadamu na kupata idhini ya kuchunguza kuhusu madai ya kuwekwa kizuizini na kuteswa kinyume cha sheria sawia na kuacha suala hili katika majadiliano ya nchi mbili ya Tanzania, Kenya, na Uganda, na kusisitiza umuhimu wa uwazi na kuzingatia taratibu za kisheria.
Karua, ambaye aliandika barua hiyo kwa nafasi yake kama mratibu wa Mtandao wa Mshikamano wa Viongozi Barani (Pan African Progressive Leaders), ametoa wito kwa mashirika hayo barani Afrika kutoa majibu yao kuhusiana na hayo ndani ya saa 72.
Haya yanajiri baada ya Mwangi kuonekana hadharani kwa mara ya kwanza siku ya Alhamisi, ambapo alidai kuwa mamlaka ya Tanzania ilimtesa kwa siku 4 hizo alizokuwa kizuizini.
By Mjomba Rashid