Mila na tamaduni vimetajwa kuchangia ongezeko la visa vya ukatili wa kijinsia pamoja na mauaji ya wanawake kaunti ya Kilifi haya yakibainika baada ya jopo linalochunguza ongezeko la visa vya ukatili wa kijinsia pamoja na ukatili dhidi ya wanawake nchini kuandaa mkao wa kutoa maoni na wakazi mjini Kilifi.
Kufuatia idadi ya visa vya ukatili wa kijinsia na mauaji ya wanawake kuongezeka kwa kasi nchini, mpango wa kimkakati unaendelea kuwekwa na jopo linalochunguza ongezeko la visa hivyo, kwa kuandaa vikao vya wakazi kutoa maoni na mapendekezo yao jinsi ya kukomesha ukatili huo.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa jopo hilo Nancy Baraza, mila na tamaduni ndicho chanzo kikubwa kinachochangia visa hivyo kaunti ya Kilifi huku akiongeza kuwa jamii imepuuza jukumu lake la kuishi kwa upendo na umoja.
Aidha amesistiza kuwa taasisi zinazoshughulikia maswala hayo zinafaa kuwezeshwa kifedha na kupewa nguvu zaidi katika kutekeleza majukumu yake.
“Tumekuwa na mkao mzuri ambao umeshuhudiwa kuibuliwa kwa hoja nyingi na wakazi wa Kilifi, na wamekuwa wawazi na kukubali kuwapo kwa changamoto za mila kuchangia ongezeko la visa vya ukatili wa kijinsia na mauaji ya wanawake. Pia wametuambia taasisi zinazoshughulikia maswala haya zinafaa kupewa mgao wa fedha wa kutosha ili kutekeleza majukumu yake inavyostahili na vile vile taasisi hizo zipewe nguvu za kutosha ili kukabiliana na visa hivyo.” alisema Bi. Baraza.
Waziri wa idara ya Jinsia kaunti ya Kilifi Dkt. Ruth Dama Masha anasema wavulana wengi wamekuwa wakihisi kutengwa na kutopewa kipaumbele katika kushirikishwa kwenye miradi mbali mbali kama vile wasichana hali anayodai imewapelekea wengi kukosa kujiamini wakati wanapotekeleza majukumu yao.
“Vijana wengi ambao wameongea leo wanahisi ni kama wametengwa na hawajashikwa mkono. Vijana hawa wanahisi akina dada wengi wamepewa kipaumbele na hizi nafasi za uongozi ni wanawake ni wanaopewa nafasi nyingi za uongozi na ushirikishwaji katika miradi mbali mbali ambapo katika katiba ya taifa letu inaelezwa kinaga ubaga kuwa nafasi zipo kwa kila mtu.
“Jambo hili pia tunaona limepunguza kujiamini kwa wavulana kwa kuwa hawajaweza kuwa na umoja na kushikana mikono wenyewe kwa wenyewe. Kwa hivyo ni sisi viongozi tunafaa tuwashike mikono hawa wavulana ndio waweze kujiamni tena katika kutekeleza majukumu yao pamoja na kujikimu katika ngazi tofauti tofauti za kimaisha.” alisema Dama.
Triza Nafula Bwire mwenyekiti wa shirika la Kilifi Civil Society ameeleza kufurahiswa kwake na kuandaliwa kwa mkao huo akisistiza kuwa kumekuwa na changamoto ya kutoa taarifa muhimu kutoka nyanjani mpaka kwa wahusika halisi kuhusu ukatili wa kijinsia na mauaji ya wanawake.
“Kulingana na sisi tunasema ni hatua tumepiga unajua ni kwasababu kwa muda mrefu unajaribu kutafuta mbinu ama taarifa muhimu kuhusu jambo nyeti ambalo linasumbua katika jamii lakini hupati hiyo nafasi. Kwa hivyo kwetu ni hatua ya kupongezwa kwa jopo hili kuja nyanjani kusikiliza mambo yanayochangia kuongezeka kwa mambo haya nay ale mapendekezo yanayoweza kupunguza kushuhudiwa kwa visa hivi katika jamii.” alisema Bwire.
Ikumbukwe rais Dkt. William Ruto aliunda jopo hilo la watu zaidi ya 40 kutafuta chanzo cha ongezeko la visa hivyo ili hatua ya kukomesha kutokea tena kwa visa ichukuliwe.
Erickson Kadzeha