Wakaazi waliofurushwa kwenye ardhi kupisha ujenzi wa nyumba za bei nafuu eneo la Likoni kaunti ya Mombasa wamelalamikia dhulma walizofanyiwa kabla ya kutimuliwa.
Wakazi hao wamedai kuwa walilazimishwa kutia saini mkataba wa makubaliano ya kupeana ardhi hiyo kinyume cha matakwa yao, lalama hizi zikiibuka baada ya kamati ya Seneti kuhusu Barabara, Nyumba na Miundombinu kuzuru maeneo hayo.
Wakiongozwa na mwenyekiti wao Jackson Maina wakazi hao wamedai kuwa hawajaekewa wazi mmiliki halisi wa ardhi hiyo ya ekari 11 iliyopaniwa kujengwa nyumba hizo tangu kuondolewa kwao miaka 2 iliyopita.
Maina amedokeza kuwa hadi kuifikia sasa fidia waliyopewa kila mmoja ni shilingi 150,000, ya kuwataka kuondoka katika ardhi, akidai kuwa makubaliano ya fidia hiyo yaliharakishwa pasi hata wao kupata muda wa kuelewa jinsi wangenufaika na mfumo wa kurejea katika makazi hayo baadaye.
Wakati uo huo wakaazi hao kupitia mwenyekiti wao huyo wamedai kutoshirikishwa kwani hakukuwa na vikao vya ukusanyaji maoni ya umma sawia na kutokuwa na uwazi kwenye mradi huo.
Wameyasema haya baada ya kukutana na kamati ya Seneti kuhusu Barabara, Nyumba na Miundombinu inayoongozwa na seneta Eddy Oketch wa kaunti ya Migori, na seneta maalum wa Mombasa Miraj Abdillahi akiwa mmoja wa mwanachama wa kamati hiyo.
Kamati hiyo ipo mjini Mombasa na mnamo Ijumaa ilizuru miradi ya nyumba za Buxton, Likoni aidha ikitarajiwa kukutana na usimamizi wa kaunti ya Mombasa pamoja na walioondolewa kwenye ardhi mbalimbali kaunti ya Mombasa kupisha ujenzi wa nyumba hizo za bei nafuu.
By News Desk