HabariLifestyleMombasaNews

Ushirikiano wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi waanzishwa Kilifi.

Mkakati wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na uhifadhi wa mazingira kwa kupanda mikoko umeanzishwa kwa ushirikiano wa taasisi za kifedha na wakazi katika wadi ya Sabaki, eneo bunge la Magarini.

Joseph Mangi, kiongozi wa shirika la kijamii la mazingira la SARICODO, anasema kupitia ushirikiano huo wameweza kufanikiwa kupanda miti 200,000 lengo likiwa ni kurejesha msitu wa mikoko ambao umepungua kutokana na kukatwa kiholela pamoja na kuongeza idadi ya samaki wanaopungua kwa kasi.

Tunanuia leo kupanda miche 200,000 ambayo kufikia mwezi mmoja ujao itakuwa imetoa majani na tunafanya hivyo kwasababu ya kurejesha misitu lakini pia tunataka kuhifadhi aina nyingine za mikoko ambazo zinapotea.

“Kwa hivyo tunavyoendelea kupanda zile aina za mikoko zinazopotea ndio tutaweza kuzihifadhi na aina zote za mikoko zitakuwa zinapatikana. Na tunafanya shughuli hii kwa manufaa ya jamii na mazingira yetu.” alisema Mangi.

Kwa upande wake ofisa mkuu wa fedha katika benki ya ABSA Yusuf Omari anasema, malengo ya upanzi wa miti milioni 10 kufikia mwaka 2032 yanaingiliana na ruwaza ya Rais ya kupanda miti bilioni 10 ifikapo mwaka uo huo wa 2032.

Tunaangalia nguzo moja ya wakfu wa ABSA ambayo inaangazia mazingira. Na tuliweka ahadi ya kupanda miti milioni 10 ifikapo mwaka 2032 na vile vile kuweza kuunga mkono serikali kufikia azma yake ya kupanda miti bilioni 10 kufikia mwaka uo huo 2032. Kwa hivyo tunajizatiti kutimiza azma yetu kwa ushirikiano na jamii.” alisema Omar

Mradi huu wa upanzi wa miti chini ya benki ya ABSA unaendeshwa katika maeneo mbali mbali katika ukanda wa pwani ikiwemo Jomvu kuu mjini Mombasa na Majoreni, kaunti ya Kwale.

Erickson Kadzeha.