Wizara ya ardhi nchini imetakiwa kuweka rekodi zote za Hati za mashamba katika mfumo wa Kidijitali ili kuepukana na Hatimiliki ghushi kutumiwa na walaghai kupata ardhi kinyume cha sheria.
Akizungumza katika kaunti ya Mombasa, Rais wa Taasisi ya Masoroveya nchini (ISK) Eric Nyadimo ameitaka wizara hiyo kuharakisha mchakato wa kusajili mashamba kidigitali ili kupunguza wizi, ulaghai na unyakuzi wa mashamba.
Kulingana naye, usajili wa mashamba kidijitali ndio “Dawa” sahihi ya kupunguza na kukomesha unyakuzi wa ardhi nchini.
“Jambo moja ambalo tunalitilia mkazo ni kuweka kumbukumbu kidigitali ili tuweze kutambua ardhi yote kiurahisi. Kwanza kabisa kipande kimoja cha ardhi hakifai kuwa na hatimiliki zaidi ya moja na iwapo kitakuwa na hatimiliki zaidi ya moja sababu ya kwanza ni ulaghai na ya pili ni kwamba hatujaweza kuweka rekodi za ardhi zetu kidigitali.
Mara nyingine ardhi inafanyiwa uchunguzi zaidi ya mara moja na kwa sababu rekodi hazijahifadhiwa vilivyo husababaisha makosa hayo.” Alisema Nyadimo.
Kwa upande wake naibu rais wa (ISK) Nelly Mbugua alisema taasisi hiyo inashirikiana kwa karibu na asasi mbali mbali zikiwemo Mahakama kuhakikisha kuna ramani za mipaka ya mashamba ili kupunguza migogoro ya mara kwa kara ya mashamba.
“Kama rais alivyosema wataalamu wetu pia wanapitia mafunzo tayari kikundi cha kwamba kiko tayari kujumuishwa kwenye njia mbadala za kusuluhisha migogoro ya ardhi ili wajuwe ni vipi kukabiliana na mipaka, masuala ya urithi na pia ni jinsi gani ya kutambua mumiliki halisi wa ardhi na pia mahakama inafanya juhudi iwezavyo kupunguza kesi za ardhi nchini.” Alisema Mbugua.
Jaji mkuu Martha Koome kupitia kwa jaji mkaazi wa mahakama kuu ya Mombasa Jairus Ngaah amethibitisha kwamba idara hiyo iko tayari kushirikiana na idara mbalimbali kukomesha unyakuzi wa ardhi na kupatikana kwa haki kwa waathiriwa.
“Tunakaribisha taasisi zote husika kushirikiana nasi ’mahakama’ kupitia kwa ushahidi wa kitaalam ama kufanya uchunguzi na pia nawataka nyinyi watalamu kukataa shughuli za kifisadi azma yetu sote inasalia kuwa kuwe kila mkenya apate ardhi kwa usawa, nathibitisha kwamba mahakama iko imara kutekeleza haki na usawa kwa wakenya wote.” Alisema Ngaah.
Wito wa Taasisi hiyo kwa wizara ya Ardhi unajiri huku migogoro ya Ardhi nchini ikiripotiwa kuongezeka hususani ukanda huu wa pwani ambako tatizo hili limekuwa kero kubwa kwa wakaazi kwa mda mrefu sasa viongozi mbalimbali wakiapa kulishughulikia swala hilo.
By News Desk