Wakazi mjini Kilifi wameshiriki maandamano ya amani kuunga mkono hatua ya kupigwa marufu uuzaji wa muguka kaunti za Mombasa, Kilifi na Taita Taveta yaliyotolewa siku kadhaa zilizopita.
Mchakato wa baadhi ya kaunti ukanda wa pwani kushikilia kuendeleza marufu ya mmea wa muguka kwa madai kuwa watumizi wa muguka kupata madhara ya kiafya, waakazi na mashirika mbali mbali yamejitokeza na kushiriki maandamano ili kuunga mkono marufuku hayo.
Kwa mujibu wa Kibibi Ali mwenyekiti wa shirika la kijamii la Kilifi Mums, utumizi wa muguka umeleta madhara mengi kuliko faida kwa wakazi ukanda wa pwani, akisistiza kuwa familia nyingi zimesambaratika, na hali ya utovu wa usalama ikiongezeka ukanda wa pwani hasa kaunti ya Kilifi.
Aidha ametaja kuwa licha ya kuanzisha mchakato wa kutaka muguka kupigwa marufuku tangu mwaka 2018, swala hili linaendeshwa kwa misingi ya siasa huku akiwarai viongozi kutilia maanani afya za wananchi badala ya kuzingatia kura.
“Mtu akipata pesa ywakimbilia muguka sasa unakuta kile kizazi kinaenda kikidimia ndio sasa viongozi wameanza kulivalia njuga swala hili. Wamejua sasa kuwa ni kweli yale waliyoyazungumza Kilifi Moms 2018 kupigwa marufuku muguka. Wamejua ni ukweli kwa maanake hivi sasa ukawapeleka vijana kwenye uwanja wakacheze mpira wengi wanaaguka na kuzimia kwasababu ya utafunaji muguka.
Wakazi mjini Kilifi wakiongozwa na Zakia Rashid na Zena Tuva wametoa wito kwa rais Dkt. William Ruto kusikiza lalama za wakazi wa pwani ambao wanadai kikazi kijacho kiko katika hatari ya kuangamia.
“Ikiwa rais William Ruto amekubali muguka uje Kilifi sisi wanawake wa Kilifi tutaenda wapi kwa maana wanaume wakioa lazima kuwe na haki ya ndoa itendeke lakini ukifika wakati huo hakuna kitu sisi kama kina mama tunakwenda wapi , je yuko tayari sisi twende huko kwao?” alisema Bi. Rashid.
“Mimi mwenyewe muguka umeniathiri sababu mwaka 2015 nilimuoza mjukuu wangu kwa harusi kubwa na baada ya kupata mtoto mmoja nguvu zake za kiume zikapotea sababu ya muguka. Mke wake akaondoka sasa ikiwa kwa sasa hivi nasubiri vitukuu je watakuja kweli?
“Wajukuu wangu ni wenda wazimu wengine hawajifai na lolote kazi yao ni kuiba sufuria wakauze ili wapate pesa wakanunue muguka. Basi twamwambia rais wetu William Ruto ajuae uchungu wa mwana ni mzazi na sisi ndio wazazi. Hatuutaki muguka huku kwetu” alisema Bi. Tuva.
ERICKSON KADZEHA.