Magavana wa kaunti za Pwani kwa pamoja wameamua kususia mwaliko wa kukutana na waziri wa Kilimo Mithika Linturi kujadili suala la marufuku ya Muguka.
Magavana hao walieleza wasiwasi wao wa tajriba ya waziri huyo wakidai kuwa hawezi kuwa kiongozi mpatanishi mwenye usawa katika suala hilo hasa baada ya kuonesha upendeleo kulingana na kauli zake za awali kuhusu Muguka.
Katika taarifa ya pamoja iliyotiwa sahihi na magavana wa kaunti 4 chini ya mwavuli wa Jumuiya ya Kaunti za Pwani (JKP) magavana wa Pwani walinukuu kauli ya Waziri Linturi akipinga marufuku ya Muguka iliyowekwa na kaunti 3 za Pwani alipoitaja hatua hiyo kuwa batili kisheria na kwamba muguka ni mmea halali wa mazao ulioratibiwa kisheria.
“Umejitokzea hadharani kutangaza msimamo wako kuhusu katiba na nafasi ya sheria ya hatua iliyochukuliwa na magavana wa Mombasa, Kilifi na Taita Taveta kupiga marufuku muguka(notisi ya gazeti la serikali 6482 ya amri ya utendaji nambari 1 ya 2024),” tarifa hiyo ya pamoja ilieleza.
Magavana hao wanne wamesema muguka si suala la kilimo bali suala la afya, maslahi mazuri na usalama wa wakazi wa Pwani na kwamba suala hilo linapaswa kushughulikiwa kwa kina na heshima pasi kuegemea upande mmoja.
“Kwa kutambua kwamba marufuku ya muguka katika kaunti za jumuiya ya pwani umezua mjadala wa kitaifa na matangazo kutoka kwa mtendaji(serikali), Idara ya Mahakama, mabunge na kaunti zote 47, tumejijazia kwamba suala hilo linamgusa zaidi mwananchi wa kawaida,” taarifa hiyo iliongeza.
Viongozi hao sasa wanamtaka rais William Ruto kusimamia mazungumzo yoyote ya mashauriano zaidi kuhusu suala hilo.
Magavana hao aidha wanaitaka Mamlaka ya kitaifa ya kudhibiti matumizi ya Mihadarati (NACADA), Wizara ya Afya, Idara za Usalama na Mashirika ya Kijamii kushiriki katika mashauriano hayo wakisisitiza kuwa marufuku ya muguka si suala la kilimo.
Kulingana na pendekezo la rais, Waziri Linturi alipaswa kukutana na viongozi wa Pwani Alhamisi hii kwenye kikao cha mashauriano kuhusu biashara hiyo ya Muguka.
BY MJOMBA RASHID