Wakazi kaunti ya Kilifi wamehimizwa kupanda miti ya matunda ili kuboresha lishe ambayo imekuwa changamoto kwa familia nyingi, pamoja na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, hayo yakijiri huku ulimwengu ukijiandaa kuadhimisha siku ya mazingira.
Juhudi za kufanyia ardhi urejesho kaunti ya Kilifi zikiendelea wito umetolewa kwa wakazi na mashirika ya kijamii kukumbatia upanzi wa miti ili kupunguza madhara yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi.
Kulingana na Winnie Masai mkurugenzi wa shirika la Inform Action wamepanda mikoko zaidi ya 600 mapema leo eneo la Mnarani huku wakifichua kushirikiana na mashirika zaidi ya 11 katika kampeni hiyo ya kupanda miti na kutoa hamasa kwa wakazi kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira.
“Tumepanda mikoko zaidi ya 600 upande wa ufuo wa Gastonia na kunayo mingine itaendelea kupandwa kesho, na tumeshirikiana na mashirika zaidi ya 11.
“Pia tunafanya kazi na vikosi vya wakazi kufanikisha mpango huo na kutoa hamasa kuhusu maswala ya uongozi kwa hivyo tunataka kuchanganya uongozi na mazingira kwasababu Kenya inasheria nzuri za utanzi mazingira ila tatizo ni utekelezwaji wake ni wakutilia shaka.” alisema Masai.
Omina Jewel ofisa wa usiano mwema wa shirika la One million trees for Kilifi, amewahimiza wakazi kaunti ya Kilifi kukomesha ukataji miti, akieleza kuwa hatua hiyo inakinga dhidi ya madhara kama vile vimbunga yanayosababishwa na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Anasema kufikia sasa shirika hilo limepanda miti zaidi ya laki moja huku likilenga kupanda miti milioni moja kaunti ya Kilifi.
“Tulivyokumbwa na kimbunga Hidaya, miti ya mikoko imetusaidia sana kupunguza madhara kwa kupunguza ile nguvu ya upepo. Ila kwasababu tunaikata kwa wingi mikoko ule upepo unapokuja tunakuta kwamba unang’oa paa za nyumba zetu, magonjwa yanashuhudiwa watoto wetu wanakufa na inatuathiri kwa ujumla.
“Kwa hivyo tunahitaji kutoa wito kwa wakazi wa Kilifi kukoma ukataji miti ambayo inaweza kufanya kaunti hii kuwa jangwa na kwa ajili hiyo tunalenga kupanda miti milioni moja kaunti hii, na tayari tumepanda zaidi ya miti laki moja.” alisema Omina.
Kwa upande wake Mercy Zawadi ofisa wa shirika la Moving The Goalpost Kilifi, amesema wameanzisha mradi wa kupanda miti ya matunda ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa lishe ambayo imewakumba wakazi wengi kaunti ya Kilifi.
“Kwenye huo mradi tumeuanza kwa kupanda miche 1,000 ya miti ya matunda kwa shule tatu ambayo ni kama yakutafiti ambapo hapo tunaangazia swala la lishe na vile vile kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.” alisema Zawadi.
Lucky Kazungu kutoka shirika la LEAF anasema ukataji miti ya asili umechangia kupotea kwa baadhi ya wadudu muhimu katika ukuaji wa miti, pamoja na vyakula kama vile uyoga.
Ameeleza kuwa kufikia sasa wamefanikiwa kupanda aina saba za mikoko kati ya aina tisa zinazopatika kaunti ya Kilifi.
“Kulingana na hii hali tunayoshuhudia mabadiliko ya tabia nchi, tunaona kwamba viumbe hai vingi ambavyo ni vya asili ya taifa hili la Kenya vimekuwa vikiharibika. Kumekuwa na watu wengi ambao wamekuwa wakihifadhi vile viumbe hai vinavyotoka mataifa ya kigeni.
“Mfano wakulima wengi wamekuwa wakipanda miti ya “Bluegam” katika mashamba yao ambayo ni miti inayoathiri sana ile ardhi na kuifanya kukosa ile uwezo wa kukuza ile miti yetu ya asili. Na utakuta kwamba inachangia kukosekana kwa wadudu muhimu wanaosaidia katika ukuaji wa miti.” alisema Kazungu.
ERICKSON KADZEHA
[…] Wakaazi Wahimizwa Kupanda Miti Ya Matunda Ili Kuboresha Lishe Kilifi June 4, 2024 […]