Kenya imejiunga na mataifa mengine ulimwenguni kuadhimisha siku ya Mazingira Duniani hii leo wito ukitolewa kwa wakazi kujukumika zaidi katika uhifadhi wa mazingira kwa maisha bora ya sasa na mustakbali wake.
Hapa nchini kaunti mbalimbali zilijumuika kuadhimisha siku hiyo kwa upanzi wa miti na uhifadhi wa mazingira kwa kusafisha fuo za bahari na miji mikuu.
Katika kaunti ya Mombasa, mashirika mbalimbali, kampuni na wanaharakati wa mazingira walishirikiana na wakazi kuadhimisha siku hii kwa upanzi wa miche sehemu mbalimbali.
Katika mazungumzo na wanahabari mnamo 6 Juni, 2024 baada ya shughuli ya upanzi wa miti na usafishaji wa mazingira katika shule ya St. Augustine huko Tudor mjini Mombasa Mwenyekiti wa Shirika la Kijamii la Clean Mombasa CBO Dakt. Mwinga Chokwe amliwataka Wakenya kuweka mazingira safi kama njia moja ya kukabiliana na maradhi tofauti yanayochipuka ulimwenguni kutokanana na uchafu.
Kulingana na Dakt. Chokwe ni kwamba usafi wa mazingira na utunzaji wa miti ni muhimu kwa afya na hasa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Aliongeza kuwahimiza wanafunzi kuepukana na utumizi wa muguka sawia na mihadarati na mingine.
“Hii miti ndio inachangia zaidi katika mambo ya tabianchi. Kusafisha hewa, kuondoa ile carbon dioxide ambayo inachafua nchi. Kadri tunavyokuwa na miti ndio joto nalo linapungua,” alisema Dakt. Chokwe.
Wakati uo huo wanafunzi wa vyuo vikuu wameapa kuendeleza ushirikiano wao na Mombasa CBO ili kushinikiza hamasisho la afya bora kupitia mazingira safi.
Kwa upande mwingine Afisa kutoka Shirika la Huduma za Wanyamapori KWS kitengo cha jamii kaunti ya Mombasa, Said Shee Mohammed, alitoa wito kwa wananchi kuchukua hatua za kukabili uchafuzi wa mazingira akitilia mkazo suala la kuwalinda wanyama na wadudu walioko hatarini kuangamia katika dunia kutokana na mabadiliko ya Tabianchi.
Afisa huyo alisisitiza kuwa jukumu la kuyalinda mazingira ni la mtu binafsi wala si la kuachiwa maafisa na idara zinazoshughulikia mazingira.
“Wakati tunakuwa na mabadiliko ya tabinchi ni kuwa si binadamu tu wanaathirika na ukame ni mpaka pia wadudu kwa sababu wanahitaji maji na wanahitaji lishe…..
licha ya kuwa tunatumia bidhaa lakini tuwe tunajua hakika hizi vitu tunazihifadhi ama uchafu wetu unahifadhiwa sehemu zinazostahili kuepuka madadhara,” alisisitiza Muhammed.
Ujumbe Mkuu wa maadhimisho ya mwaka huu ni ‘Kufanyia ardhi urejesho, hali ya jangwa, na Kustahmili ukame, chini ya kauli mbiu Ardhi Yetu, Mustakbali Wetu.’
Maadhimisho ya Kimataifa ulimwenguni yalifanyika nchini Saudi Arabia.
Pia unaweza pitia;
BY EDITORIAL DESK.