Viongozi wa kidini Kaunti ya Mombasa sasa wamelalamikia hatua ya polisi kutumia nguvu kupita kiasi kukabiliana na waandamanaji vijana barubaru maaarufu Gen Z ambao hawakuwa na silaha.
Hii ni baada ya kijana Rex Kanyike Masai kuuawa kwa kupigwa risasi jijini Nairobi wakati wa maandamano ya kupinga Mswada tata wa Fedha wa 2024.
Katibu Mkuu wa Baraza la Maimamu na Wahubiri Nchini CIPK, Balozi Sheikh Mohammad Dor, alieleza maskitiko yake kufuatia kitendo hicho ambacho alikikashifu na kuibua maswali kwa nini askari walitumia nguvu kuwakabili waandamanaji hao.
Akizungumza na Wanahabari mnamo Ijumaa Juni 21, Sheikh Dor aliwapongeza vijana kwa kuandaa na kushiriki maandamano hayo pasi kushuhudiwa vurugu zozote, akisema maandamano hayo ya vijana wa Kizazi cha Z (Gen-Z) yaliandikisha historia nchini kwa kuwa maandamano ya amani kuwahi kushuhudiwa.
“Kwa nini polisi atumie nguvu na kupiga risasi waandamanaji ambao hawajajihami, hawakuwa na silaha yoyote, ila tu simu zao, maji na maski? Sote tuliona Mombasa, Kilifi, Nairobi hata Eldoret na kwingine maandamano yalikuwa ya amani na utulivu. Na nawapongeza vijana wa Gen Z, kwa kuongoza maandamano ya amani kabisa Katika historia ya Kenya haya ni maandamano ya amani zaidi kuwahi kushuhudiwa na inaskitisha kuona askari wanayatibua na hata kumpiga risasi kijana Masai. Sisi CIPK tunakashifu vikali.” Alisema Sheikh Dor.
Katika ukanda wa Video unaosambaa mtandaoni umeonesha polisi ambaye hakuwa amevalia sare rasmi za kazi mnamo jioni ya Alhamisi Juni 20 akimpiga risasi kiunoni kijana huyo na kuanguka na japo kijana mwenziwe alimsihi askari huyo amsaidie kumbeba kumfikisha hospitalini kwa matibabu. Kulingana na rafikiye Masai, askari huyo alikataa na kusema ‘acha akufe.’
Akilaani vikali kitendo hicho cha polisi, Sheikh Dor ambaye alikuwa Balozi wa Kenya nchini Oman aliilaumu idara ya polisi na akashinikiza uchunguzi wa haraka ufanywe na hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya askari aliyetekeleza mauaji hayo.
Sheikh Dor aidha alimtakia afueni ya haraka askari aliyejeruhiwa katika maandamano ya siku ya Jumanne yaliyofanyika katikati ya jiji la Nairobi.
“Tunasikitika sana kwa hilo na kama Baraza tunawaambia serikali uchunguzi ufanywe haraka polisi huyo ajulikane na achukuliwe hatua, na vile vile pia tunatuma risala zetu za pole kwa askari aliyepoteza mikono yake miwili kwa kulipukiwa na kitoa machozi, tunamtakia afueni ya haraka.” Alisema Balozi Dor.
Wakati uo huo Sheikh Dor ambaye aliwahi kuwa Mbunge Maalum alimrai rais William Ruto kuchukua hatua kama kiongozi wa taifa kutuliza joto nchini kutokana maandamano yanayoendelezwa na vijana hao.
Alisema hatua ambayo vijana hao wamechukua inaashiria pengo lililopo katika sera za serikali na hivyo kuna haja kuwe na mbinu mwafaka ya kuhakikisha kilio na maoni ya vijana yanasikilizwa.
“Twamuomba rais asipuuze haya yanayoendelea, awasikilize hawa vijana maana maandamano wanayofanya bila shaka wanawakilisha wazazi wao wanaopitia ugumu wa maisha, wanawakilisha wengi na wao vijana wenyewe pia wameona mswada wa fedha utapelekea maisha kuwa magumu zaidi ukipitishwa.” Alisema Sheikh Dor.
Katibu Mkuu huyo wa CIPK aidha aliisihi Serikali iachane na mswada huu wa sasa akieleza haja ya kutumiwa sheria ya fedha iliyopita ya mwaka 2023 badala ya kuleta sheria mpya ambazo zitamuumiza zaidi Mkenya.
Alisema licha ya kuwa ni sharti mswada wa fedha upendekezwe na kupitishwa kuwa sheria kila mwaka, si lazima serikali iongeze mzigo wa ushuru zaidi kwa mwananchi ambaye tayari anazidi kuzongwa na gharama ya maisha.
“Ile bill iliyopitishwa 2023 twaiambia serikali iweze kutumia ile ile bila kuongeza uzito tena kwa wananchi. Ikiwa ni lazima maana tunajua lazima Serikali ikisoma bajeti iandamane na mswada wa fedha lakini inaweza kupunguzwa au kutumiwa ile ile iliyopita. Tunatoa nasaha kwa Serikali mambo mawili yanaweza ikufanywa kwa nia ya kuipenda hii nchi yetu, Serika ituhakikishie kuwa ufisadi utaweza kuondoka na ubadhirifu uweze kuondoka pia.” Alisema Sheikh Dor.
Haya yanajiri huku tayari Mswada huo ukipitishwa katika awamu ya kwanza uliposomwa kwa mara ya pili Bungeni mnamo Alhamisi Juni 20, ambapo wabunge 204 walipiga kura ya NDIO kuunga mkono na huku wabunge 115 wakiupinga Mswada huo.
Hata hivyo maandamano zaidi yanatarajiwa kuanzia Jumatatu wiki ijayo kabla ya Mswada huo wa Fedha 2024 kusomwa kwa mara ya mwisho na kisha Kupigiwa kura ya kupitishwa kuwa sheria au kuangushwa mnamo Jumanne, Juni 25.
BY MJOMBA RASHID