HabariNews

Maseneta na Wabunge Waisuta SRC kwa Kuwapa Nyongeza ya Mshahara

Maseneta na wabunge wamejitokeza kuisuta Tume ya Kutathmini Mishahara na Marupurupu ya  Umma, SRC kufuatia tangazo lake la kuongeza mishahara kwa maafisa wa ngazi za juu serikalini.

Wakizungumza katika kikao cha Jumatano cha Bunge la Seneti, Seneta wa Kilifi aliye pia Naibu kiongozi wa wachache Stewart Madzayo amesema binafsi yeye hahitaji nyongeza hiyo ya mishahara kwa sasa Wakenya wakiendelea kulalamikia gharama ya maisha.

Seneta wa Kilifi, Stewart Madzayo amesema binafsi yeye hahitaji nyongeza hiyo ya mishahara kwa sasa Wakenya wakiendelea kulalamikia gharama ya maisha.

“Bwana Spika mimi nasema sitaki mshahara wangu uongezwe, ilikuwa sisi tupewe na najua ndugu zangu maseneta tuko hapa tuna shida za pesa kweli, ila si wakati mzuri kuongezewa mshahara. Tumekataa.” Alisema.

Madzayo aliye pia Naibu kiongozi wa wachache katika Bunge la Seneti, amesema si wakati mwafaka kwa sasa maafisa wowote serikalini kuongezewa mshahara akisema ni vyema nyongeza hiyo ikaelekezwa kupewa wakenya walio na shida na walioathirika kwenye maandano.

“Mshahara huo kwa sasa ukae kando wapewe ambao hawajiwezo waweze kuendelea na maisha kisawasawa ama hii pesa ipelekwe wale walipata majeruhi ama waliofariki wale na shida zao ziende huko kuwasaidia.” Alisema Madzayo.

Ni Kauli iliyoungwa mkono na Seneta wa Nairobi aliye katibu wa Chama cha ODM Edwin Sifuna aliyesema hakuna Seneta aliyeitisha nyongeza hiyo na ni kinaya ikikumbukwa kuwa wakenya wanalilia gharama ya juu ya maisha na matozo ya juu ya ushuru.

Na ninafurahi vile maseneta wenzangu waaliotangulia kuzungumzia hili, hakuna aliyehitajia nyongeza hiyo, binafsi sikuitisha nyongeza hiyo ya elfu 14, naunga mkono pendekezo la maseneta waliosema tuamue kama Seneti kuwa hatuna haja na nyongeza yoyote ya mshahara katika mwaka huu wa kifedha.” Alisema.

Kwa upande wake Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino amesema wabunge na maafisa wengine sarikalini hawafai kuongezewa hata shilingi wakati huu uchumi wa taifa ukiwa umedorora.

Kulingana na SRC Wabunge na maseneta sasa watapokea shilingi 739,600 kila mwisho wa mwezi, huku Maspika Moses Wetangula wa Bunge la Kitaifa na Amason Jeffa Kingi wa Seneti wakipewa nyongeza ya shilingi milioni 1.2 na marupurupu mengine.

Hii ni licha ya wimbi la maandamano ya Wakenya kuiipinga serikali kwa madai ya ufisadi, utumizi mbaya wa raslimali na mishahara mikubwa wakati ugumu wa maisha ukiwazonga.

BY MJOMBA RASHID