Ukosefu wa uwekezaji wa kijamii yaani “Social Harvesting” umetajwa kuchangia kwa kiwango kikubwa ukosefu wa ajira, ikibainika kuwa vijana wengi humu nchini wamelazimika kufanya vibarua tofauti na taaluma walizosomea.
Changamoto ya ukosefu wa ajira ikiendelea kutajwa kuwa kikwazo katika ukuaji wa uchumi humu nchini, imebainika kuwa licha ya vijana kusomea taaluma mbali mbali hawajafanikiwa kujiimarisha kimaisha.
Akizungumza kwenye warsha ya mradi wa USAWA iliyoandaliwa mjini Kilifi na shirika la wanahabari wanawake nchini AMWIK, Shamsa Abubakar Fadhil, maarufu “Mama Shamsa” kutoka baraza la kidini nchini, amesema wazazi wamewekeza kwa elimu ya watoto wao ila hawajapata faida ya uwekezaji huo.
Amesistiza kuwa wazazi wanahisi kupoteza raslimali zao kuwasomesha watoto wao na kisha kukosa ajira.
“Sisi wazazi tunawekeza kwa elimu ya mtoto lakini hatupati majibu hakuna “social harvesting” imepotea ndani ya Kenya na kama mzazi inauma.
“Mimi nasomesha mtoto wangu mpaka chuo kikuu halafu anaishia kuwa dereva wa tuk tuk, anaishia kuwa dereva wa taxi, anafanya biashara ya kuuza ndizi sokoni, ni kama elimu iko lakini ni kama hufanyii kazi ile elimu ambayo umesomea. Huo ni upotezaji mkubwa wa raslimali.” alisema Mama Shamsa.
Aidha ameitaka serikali kuhakikisha kuwa inatekeleza jukumu la kuunda nafasi za ajira ili kutatua changamoto hiyo akiongeza kuwa viongozi kushikilia wadhifa mmoja serikalini kutasaidia kuhakikisha kuwa kuna ugavi sawa wa nafasi za ajira.
Amesistiza kuwa mbinu hiyo pia itasaidia kukabiliana na ulaghai, kupotea kwa raslimali na kushambuliana yaani (Fraud, Waste, Assault) FWA.
“Ni jukumu la serikali kuhakikisha kuwa wameweka mikakati ya kuhakikisha hawa watu wanapata ajira. Mtu mmoja ambaye amepitisha umri wa kustaafu kushikilia nyadhifa zaidi ya tano inavunja moyo.
“Wewe unapoteuliwa kuwa waziri basin i ubaki kuwa waziri ili hizi kazi ziwe na mgao. Jambo jengine mimi nimesafiri sana na nikuwa hatuwekezi kwa njia mbadala za ujuzi wa kimaisha kwa vijana wetu, tunawafunza kupata kazi za ofisini.” alisema Mama Shamsa.
BY ERICKSON KADZEHA