HabariNews

Aliyekuwa Waziri wa Utalii Najib Balala Aondolewa Mashtaka ya Ufisadi wa Bilioni 3.3

Idara ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtakaya Umma nchini, ODPP mapema Jumatano Julai 31, imeondoa mashtaka ya ufisadi dhidi ya aliyekuwa Waziri wa Utalii nchini Najib Balala na wenzake 16.

Kulingana na idara hiyo ushahidi uliowasilishwa na Tume ya Maadili na kupambana na Ufisadi hautoshi kushtaki maafisa hao 17 wa wizara ya Utalii.

Kufuatia hilo, Mahakama ya Malindi ilikubali ombi la Mwendesha Mashtaka, DPP kusitisha kesi hiyo na kumwondolea mashtaka ya ufisadi yaliyokuwa yakimzonga Balala katika sakata ya shilingi bilioni 3.3 ya Chuo cha Utalii.

Hata hivyo akitoa uamuzi wa kesi hiyo hakimu mkuu katika mahakama ya Malindi, James Mwaniki alisema kesi hiyo huenda ikarudishwa mahakamani endapo tume ya EACC itapata ushahidi zaidi.

Akizungumza baada ya kutolewa Kwa kesi hiyo wakili wa Balala ameilaumu idara ya mashtaka akisema inafanya uchunguzi duni kabla kuwasilisha kesi mahakamani.

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi EACC kwa sasa italazimika kutafuta ushahidi zaidi dhidi ya maafisa hao kuhusu ufujaji wa fedha za ujenzi wa chuo Cha Utalii kilichoko kaunti ya Kilifi.

By Joseph Yeri